MWILI WA MTANGAZAJI ISACK GAMBA KUWASILI TANZANIA KESHO


Marehemu, Isack Gamba enzi za uhai wake.

Mwili wa aliyekuwa mtangazaji wa zamani wa ITV, Radio One na baadaye Idhaa ya Kiswahili ya DW, Isack Muyenjwa Gamba utawasili kesho Alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Mwili huo utawasili Jumatatu Oktoba 29,2018 saa nane alfajiri kutoka nchini Ujerumani, ukisindikizwa na mtangazaji Sudi Mnete.

Kupitia taarifa iliyotolewa na mmoja wa wanafamilia ya Gamba, mwili huo utapokelewa na kupelekwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo ambako ibada na shughuli nzima ya kumuaga kwa heshima zote itaanza saa tano asubuhi siku ya Jumatatu na baadaye utapelekwa uwanja wa ndege tayari kwa safari kuelekea kwao Bunda kupitia Mwanza kwa ajili ya maziko.

"Baada ya kuwasili jijini Mwanza, wadau wa mbalimbali watapata nafasi ya kuuaga mwili wa Gamba kuanzia saa tano asubuhi siku ya Jumanne, Oktoba 30, katika viwanja vya ofisi za umoja wa vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC) vilivyopo Isamilo, na baadaye msafara wa magari utaondoka kuelekea Bunda", imesema taarifa.

Taarifa juu ya kifo cha mtangazaji huyo nguli wa zamani zilisambaa usiku wa Oktoba 18, zikieleza kuwa alikutwa akiwa amefariki nyumbani kwake mjini Bonn Ujerumani ambapo kabla ya kubainika kwa kifo chake mtangazaji huyo hakuonekana ofisini kwa takribani siku tatu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post