FC BARCELONA:WATAWEZA BILA MESSI LEO??



Meneja wa klabu bingwa nchini Hispania FC Barcelona Ernesto Valverde amekitaka kikosi chake kujifunza kupambana bila ya nahodha na mshambuliaji Lionel Messi, ambaye atakosa baadhi ya michezo, kufuatia kupata jeraha la mkono mwishoni mwa juma lililopita, wakati wa mchezo wa La Liga dhidi ya Sivilla CF.

Valverde ametoa tamko la kuwahimiza wachezaji wake kujenga ujasiri wa kucheza bila Lionel Messi, alipokua katika mkutano na waandishi wa habari uliozungumzia mpambano wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi, ambao utawakutanisha dhidi ya Inter Milan, leo usiku kwenye uwanja wa Camp Nou.

meneja huyo aliejiunga na FC Barcelona msimu wa 2017/18 amesema, kuna ulazima wa wachezaji wake wakajitambua na kuamini hakuna mchezaji zaidi ya klabu, na kama watakua na mawazo ya kumtegemea Messi, watakua wanakosea.

“Tunapaswa kushirikiana kwa pamoja, mmoja wetu anapoumia ama kuwa na matatizo mengine ya kimaisha, hatuna budi kujiamini na kuendeleza mapambano dhidi ya adui zetu,” alisema Valverde.

“Tuna wachezaji wengi wenye uwezo wa kuziba pengo la Messi, ninaamini katika mchezo wetu dhidi ya Inter Milan mtaliona hilo, kuumia kwa mshambuliaji huyu sio mwisho wa mapambano, tutaendelea na tutahakikisha tunapigania alama tatu muhimu.”

FC Barcelona, ambao walishindwa kuendelea na michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita baada ya kufungwa na AS Roma katika mchezo wa robo fainali, msimu huu wameanza vyema kwa kuzichapa Tottenham na PSV, hali ambayo inawafanya kuongoza msimamo wa kundi B, wakiwa na alama sita sawa na Inter Milan, lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, inawaweka juu mabingwa hao wa Hispania.

Hata hivyo usiku wa leo FC Barcelona watakua na kazi ya kufanya kufuatia wapinzani wao (Inter Milan) kuwa na muendelezo mzuri katika michezo waliyocheza siku za karibuni, kwani mpaka sasa wamecheza michezo saba bila kupoteza hata mmoja.

Kufuatia hali hiyo, Valverde aliwaambia waandishi wa habari kuwa: “Inter Milan ni moja ya klabu kubwa barani Ulaya na ina wachezaji wazuri, sishangazwi na muendelezo wao mzuri wa kushinda michezo saba mfululizo. Wana tabia ya kutokukata tamaa, lakini naamini vijana wangu leo watapigana ili kuwapa upinzani wa kweli.”

Taarifa za timu zote mbili (FC Barcelona Vs Inter Milan)

Inter Milan watamkosa kiungo kutoka nchini Ubelgiji Radja Nainggolan, Marcelo Brozovic na Ivan Perisic, ambao ni majeruhi.

Nainggolan aliumia wakati wa mchezo wa ligi ya Italia mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya AC Milan, hali kadhalika kwa Ivan Perisic ambaye alilazimika kutolewa katika mchezo huo uliomalizika kwa Inter Milan kuchomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Meneja wa Inter Milan Luciano Spalletti amesema, kiungo Nainggolan mwenye umri wa miaka 30, hatoweza kucheza dhidi ya FC Barcelona kutokana na jeraha la kifundo cha mguu, ambalo alilipata kufuatia rafu aliyochezwa na Lucas Biglia wa AC Milan.

Kwa upande wa FC Barcelona mabeki Samuel Umtiti na Thomas Vermaelen wataendelea kuwa nje, kutokana na majeraha yanayowakabili, hali kadhalika kwa Lionel Messi anaeuguza jeraha la mkono.

Beki wa kushoto wa FC Barcelona Jordi Alba amesema: “Kumpoteza Messi katika michezo kadhaa ni hasara kubwa kwetu, kwa sababu tumezoea kucheza kwa pamoja na wakati mwingine tunafurahishwa na uwajibikaji wake anapokua uwanjani, tutajitahidi kupambana bila yeye, na nina uhakika tutashinda.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527