DAWA YA VIWAVI JESHI VAMIZI VYA MAZAO YAPATIKANA

Na Hellen Kwavava - Dodoma

Asilimia 80 ya Utafiti wa mbegu ya mahindi iliyowekwa vinasababa unaofanywa katika kituo cha Utafiti wa Kilimo Makutupora Mkoani Dodoma(TARI) umeonyesha kuwa na uwezo wa kuhimili mdudu aina ya Kiwavi jeshi vamizi ambaye anashambulia katika zao la mahindi kwa kasi kubwa nchini.

Lakini pia asimilia 100 ya Utafiti huo ambao uko mbioni kukamilika unaonyesha kuwa na uwezo wa kumhimili mdudu aina ya Bungua ambaye pia amekuwa tishio katika zao hilo la mahindi.

Hayo yamebainishwa na Mtafiti Mkuu wa Mbegu hiyo ya Uhandisi Jeni(GMO) kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Makutupora mkoani Dodoma Dkt. Justin Ringo wakati akitoa ufafanuzi wa mbegu hiyo kwa Wakulima pamoja na waandishi wa habari waliopata fursa ya kutembelea kituo hicho na kujionea Utofauti uliopo wa Mahindi yaliyopandwa na mbegu iliyowekewa vinasaba hivyo na ile mbegu chotara ambayo inatumiwa na wakulima kwa sasa.

“Kama watafiti tuliofanya hili jaribio tumejionea kabisa Teknolojia hii ya Uhandisi Jeni umefikia lengo kwa asilimia 80 ya wadudu viwavi jeshi vamizi na asilimia 100 kwa wadudu aina ya Bungua ukitofautisha na mbegu chotara ambayo tumejionea kwa msimu wa kilimo uliopita wadudu wameweza kushambulia zao la mahindi kwa wingi jambo ambalo limeleta hasara hata kwa serikali”,Dkt Ringo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Amos Ningu ameeleza kuwa majaribio kama haya wanayofanya yanasaidia kumkomboa mkulima ili kuweza kunufaika na kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo lakini pia kusaidia zaidi usalama wa chakula katika taifa.

“Kama Tume ni jukumu letu kubwa kufanikisha utafiti wa Teknolojia kusudi tuone kama unatatua changamoto zilizopo katika kilimo ili tuishauri serikali na kama itaridhia tuweze kuifaulisha,Lakini bado wadau wengine wanaruhusiwa kuja kuiona Teknolojia hii ili kuweza kuondoa mashaka ambayo wanaweza kuwa nayo katika Teknolojia hii”,alisema Ningu.

Nao wakulima waliofanikiwa kujionea hiyo teknolojia na waliiomba serikali kuweza kuangalia utafiti huo uliofanyika katika Kituo hicho kwa kina ili kuweza kuruhusu mbegu hizo ziweze kuwafikia,Farida Ally na Thomas Nile wameeleza kufurahishwa na mbegu hiyo na kusema kwamba hasara waliyopata msimu uliopita wanaomba serikali kuwaangalia ili kuweza kunufaika na kilimo chao.

“Msimu wa kilimo uliopita nililima ekari mbili za mahindi lakini nimevuna gunia mbili tu tofauti na Gunia 8 zilizopita na hiyo imetokana kuvamiwa na hawa wadudu”,alisema Farida.

“Mahindi ni kilimo changu kikuu lakini nimeamua kuacha kwa sasa kutokana na wadudu hawa kunipa hasara kubwa sana,Tumejionea hapa na kuridhik na mbegu hii tunaiomba serikali kuiruhusu mbegu hii kuingia sokoni ili tunufaike nayo”,aliongeza Nile.

Utafiti huo wa Teknolojia ya Uhandisi Jeni(GMO) unatarajia kumaliziaka mwezi Desemba kwa kuvunwa na ulihusishwa Jini mbili ambayo moja ilihusu upande wa Wadudu na nyingine iliangalia namna ya kuhimili ukame.
Dkt. Justin Ringo Mgunduzi wa mbegu hiyo akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kwenye shamba la majaribio Makutupora Dodoma.
Mdudu  Kiwavi jeshi
Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti Makutupora Dodoma Dkt Cornell Massawe akionesha mahindi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post