Picha : WANAFUNZI WANUSURIKA KIFO KWA KUTUMBUKIA CHOONI SHULE YA MSINGI SELIANI ARUSHA


Kikosi cha uokoaji kikiendelea na zoezi la kufukua kifusi katika choo kilichotitia, shule ya msingi Siliani.

Wanafunzi wa Shule ya msingi ya Seliani jijini Arusha wamenusurika kifo baada ya choo cha shule hiyo kutitia na kuibua taharuki kwa wazazi, ambapo mtoto mmoja ameripotiwa kupata majeraha na anaendelea na matibabu katika hospitali ya Seliani.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru iliyopo mkoani humo, Jerry Murro amesema kuwa tukio hilo limetokea asubuhi majira ya saa 4, ambapo mwanafunzi mmoja amejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya wilaya.

Muro amewataka wananchi kuwa watulivu wakati wa zoezi la ufukuaji wa vifusi vilivyoporomoka katika choo hicho ili waweze kuona kama kuna wanafunzi wengine wamefukiwa ingawa inasemekana walikuwa zaidi ya mmoja ndani ya choo hicho.

"Tayari kikosi cha uokoaji kinaendelea na kazi ya kutoa vifusi ili kuangalia kama kuna wanafunzi wengine waliofukiwa, na baadaye tutaunda tume ya uchunguzi wa tukio hili ili kufahamu chanzo", amesema Muro.

Kutokana na shule hiyo kuwa na choo kimoja chenye matundu ishirini ambacho ndicho kilikuwa pekee kwa shule hiyo, imemlazimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuchukua hatua za kuzungumza na uongozi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Seliani na kuomba shule kutumia vyoo vya Kanisani hilo, ombi ambalo lilikubaliwa na Mkuu wa jimbo la Arusha Magharibi, Mchungaji Philemon Joseph Mollel ambae aliungana na Mkuu wa Wilaya katika zoezi la uokoaji na hivyo kuondoa mashaka ya kufungwa kwa shule hiyo.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI  KUHUSU TUKIO LA KUTITIA KWA CHOO KATIKA SHULE YA MSINGI SELIAN ARUMERU

Leo 26/10/2018 Majira ya Saa tatu na nusu asubuhi tumepata changamoto ya kutitia na kuanguka kwa Jengo la choo cha shule ya Msingi ya Seliani katika kijiji cha Olevolosi kata ya kimnyaki Wilaya ya Arumeru ambapo katika tukio hilo tumeweza Kuokoa Mwanafunzi Mmoja wa Kiume aliepata majeraha sehemu na bado tunaendelea na jitahada za kuondoa kifusi kilichochanganyikana na matofali ambacho kimezama katika Shimo la choo kilichokuwa na matundu 20


Katika kukabiliana na Changamoto Iliyotokea Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Jerry Muro akiambatana na Katibu Katibu tawala wa Wilaya na viongozi wa Halmashauri ya Arusha walifika kwenye eneo la tukio na kuanza kazi ya kuratibu jitihada za  uokoaji wakishirkiana na vikosi vya uokoji na Zimamoto pamoja na mamia ya wananchi wa kata ya kimnyaki ambapo walifanikiwa kumuokoa mwananfunzi Mmoja akiwa amejeruhiwa usoni na kukimbizwa katika hospital ya Seliani kwa matibabu zaidi ambapo mpaka sasa vikosi vya uokoaji vinaendelea na jitihada za kufukua kifusi pamoja na matofali yaliyozama katika choo hicho Cha shule chenye matundu 20 ambacho ndio choo pekee Kinachotumiwa na zaidi ya wanafunzi 1,121 wa shule hiyo.


Katika Eneo la tukio kwanza tulilazimika kurejesha hali ya Amani na kutuliza taharuki za wananchi ambao baadhi Wana watoto wanaosoma katika shule hiyo na kutoa nafasi kwa vikosi vya ukoaji kuendelea na zoezi la kutafuta wanafunzi wengine Kutokana na kutokupatikana kwa Taarifa za awali zinazoonyesha idadi ya Wanafunzi ambao huenda walikuwa kwenye choo hicho.


Kutokana na shule hiyo kuwa na choo kimoja chenye matundu ishirini ambacho ndicho kilikuwa pekee kwa shule hiyo ilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuchukua hatua za kuzungumza na Uongozi wa Kanisa la KKKT usharika wa seliani na kuomba shule kutumia vyoo vya Kanisani ombi ambalo lilikubaliwa na *Mkuu wa jimbo la Arusha Magharibi Mchungaji Philemon Joseph Mollel ambae aliungana na Mkuu wa Wilaya katika zoezi a uokoaji na hivyo kuondoa Mashaka ya kufungwa kwa shule.


Kutokana na kadhia hiyo ilimlazimu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe Jerry  Muro kuzungumza na wananchi waliojitokeza ambapo katika mazungumzo yake aliwataka wananchi kutulia na kutoa fursa ya kuendelea kwa zoezi la utoaji wa kifusi ili kujirisha na madhara zaidi ambayo huenda yametokea.


Awali kwa upande wao baadhi ya wananchi waliungana na Mkuu wa Wilaya katika kuchanga Fedha kwa ajili ya kuanza Mikakati ya Ujenzi wa choo kingine ili kutokwamisha masomo ya wanafunzi kazi ambayo ilifanywa na Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wa Kanisani na halmashauri na kuitikiwa kwa wingi na wananchi waliotoa Fedha zao.


Awali Mhe Muro alilazimika kumtembelea majeruhi ambae amelazwa katika hospitali ya seliani na kumjulia hali uku akiongozana na viongozi mbalimbali.


Imetolewa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru

26/10/2018
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post