CAPE VERDE YAICHAPA TAIFA STARS 3-0

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' jana usiku kimekubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Cape Verde na sasa kitalazimika kuanza kupiga mahesabu ya mataifa yaliyopo kundi L ili kuona kama kinaweza kufuzu fainali za AFCON 2019 nchini Cameroon.

Tanzania imepokea kichapo hicho ugenini katika mchezo ambao ni wa tatu katika kundi L, lenye timu za Tanzania, Uganda, Lesotho na Cape Verde. Tanzania sasa imebaki na alama 2 katika nafasi ya 3 huku Cape Verde wakienda kileleni kwa kufikisha alama 4.


Tanzania sasa itaanza kusubiri matokeo ya wapinzani wake ikiwemo Uganda wenye alama 4 kwenye mechi mbili ambao leo wanacheza na Lesotho yenye alama 2 baada ya mechi 2 ikiwemo alama moja waliyopata hapa nchini kwa kutoka sare na Tanzania kwenye mechi ya kwanza ya kundi hilo.


Timu za Uganda na Lesotho kila moja ina nafasi ya kuongoza kundi hilo endapo itashinda katika mchezo wa leo ambao utapigwa nchini Lesotho. Uganda wakishinda watafikisha alama 7 na kurudi kileleni lakini Lesotho nao wakishinda watafikisha alama 6 na kupaa kileleni.


Baada ya mchezo wa jana Tanzania na Cape Verde zitarudiana Jumanne Oktoba 16, 2018 jijini Dar es salaam. Mabao ya Cape Verde yamefungwa na Gomes Ricardo dakika za 16 na 23 pamoja na Ianique Tavares dakika ya 85.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post