ANAYEDAIWA KUWA JAMBAZI SUGU AKAMATWA MWANZA


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Jonathan Shana.

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limefanikiwa kumtia nguvuni mtu mmoja aitwaye Peter Thomas Nyanchiwa, anayedaiwa kuwa jambazi sugu, akiwa ameiba gari na kutaka kutoroka nalo kwenda kuliuza nchini Uganda.

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo na wenzake wawili, waliiba gari aina ya Toyota Costa lenye namba za usajili T 122 DLY mali ya Ismail Abdallah mkazi wa Mwanza.

Siku ya tukio la wizi huo inadaiwa mtuhumiwa akiwa na wenzake wawili walikodi gari hilo kuelekea Serengeti kwa madai ya kubebea watalii waliokuwa wameharibikiwa gari njiani wakati wakiendelea kutalii. 

Ismail Abdallah alikubaliana nao na kuanza safari hadi walipofika eneo la Nata Serengeti ambapo mtuhumiwa na wenzake walimbadilikia na kumfyatulia risasi ya kwenye taya na kudondoka chini na watuhumiwa kuamini kuwa tayari wamemuua. 

Baada ya kutekeleza tukio hilo walianza safari ya kuelekea Mkoani Geita kwa kupitia barabara ya Bariadi, Shinyanga hadi Kahama kwa lengo la kulipeleka gari hilo nchini Uganda kwa ajili ya kuliuza. 

Taarifa za wananchi kwa jeshi la polisi zilisaidia kufanyika kwa msako na kufanikiwa kukamata gari hilo katika eneo la Runzewe mkoani Geita pamoja na Bastola yenye namba H44780Y ikiwa ana risasi 12 ndani ya magazine.

Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokamilika. Hali ya Ismail Abdallah imeelezwa kuwa inaendelea kuimarika baada ya wananchi kumkimbiza katika hospitali ya wilaya ya Serengeti kwaajili ya matibabu
Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post