YALIYOJIRI KWENYE MNADA WA MAKONTENA YA MAKONDA LEO DAR


Mnada wa mali zilizomo ndani ya makontena 20 ya yaliyoandikishwa kwa jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, umeendeshwa na tayari wateja baadhi wamekagua bidhaa kwa ajili ya kununua lakini wameshindwa kufika bei iliyotakiwa na mamlaka ya mapato nchini (TRA).

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayohusika na kuendesha minada ya Yono Auction Mart, Scholastica Kevela Yono, amewaambia waandishi wa habari kuwa kuna matumaini ya bidhaa zote kununuliwa tofauti na mnada wa awali uliokosa wateja kabisa lakini leo baadhi wameweza kununua na mnada mwingine utaendeshwa Jumamosi ijayo Septemba 8.


Akiendesha mnada huo Kevela amezitaja bidhaa zilizomo kwenye makontena hayo ni samani za ofisini kama vile viti, meza na makabati, huku bei zilizotajwa ni kati ya Shilingi milioni 6 hadi milioni 15 huku akibainisha kuwa mnada huo umehusisha sio makontena ya Mhe. Makonda pekee yake bali na makontena mengine ambayo yameshindwa kulipiwa ikiwemo vifaa vya kilimo pamoja na magari.

Mnada huo umefanyika katika bandari kavu ya Malawi Cargo na wanunuzi wametakiwa kuwa na vitambulisho, leseni ya gari na hati ya kusafiria.

Makontena hayo yanapigwa mnada baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, kuagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Makonda, yapigwe mnada ikiwa ni sehemu ya kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.


Mbali na Makonda mwenyewe kutoridhia uamuzi huo wa serikali, tayari Rais Dkt. Magufuli amesema sheria za nchi zinasema wazi kuwa ni mtu mmoja tu katika nchi mwenye dhamana ya kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.


Rais Magufuli amesema kuwa hakuna mtu mwingine zaidi ya aliyeruhusiwa kwa mamlaka aliyopewa, “Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako, halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, Maana yake nini?”.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527