WAZIRI MKUU: ULAJI USIOFAA UNAONGEZA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema lishe duni pamoja na ulaji usiofaa na mitindo ya maisha vinachangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususan kwa vijana na watu wazima, ambao ndiyo nguvu kazi kwa Taifa.“Ni jambo lisilopingika kuwa hatua za kukabiliana na magonjwa ya kusendeka (mfano matatizo ya moyo, saratani, kisukari na shinikizo kubwa la damu) zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kasi ya maendeleo yetu kwani gharama za matibabu yake ni kubwa mno; si kwa kaya zinazoathirika tu bali kwa Taifa zima.”


Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 11, 2018), wakati akifungua mkutano wa tano wa wadau wa masuala ya lishe, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kambarage, Hazina jijini Dodoma. 


Waziri Mkuu amesema lishe iliyozidi inadhihirishwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukizwa yanayotokana na mabadiliko ya mitindo ya maisha na ulaji usiofaa kama vile uzito uliozidi, viriba tumbo, shinikizo la damu pamoja na kisukari.


Amesema kasi ya ongezeko la magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza inapaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha. “Huu ni wakati wa kuangalia kwa pamoja kama jitihada zetu zinaleta matunda tunayotarajia.”


Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya Taifa letu hivyo, uwepo wao katika mkutano huo unaonesha umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa kila sekta, kila mdau ikiwemo sekta binafsi kwa nafasi yake katika kupambana na aina zote za utapiamlo. 


Amesema ushiriki wa kila sekta ni wa muhimu kwa sababu hakuna sekta moja pekee inayoweza kuondoa tatizo la utapiamlo, pia ni vema kwa wadau hao wakajitathmini mmoja mmoja katika sekta zao kuona kama wanaelekea katika muelekeo sawa na mipango ya Serikali.


“Kwa kuzingatia hilo, ofisi yangu imeweka utaratibu maalum wa kuratibu utekelezaji wa kazi za lishe nchini, ambapo kamati ya Kitaifa ya Usimamizi na Ushauri kuhusu masula ya lishe nchini yaani High Level Steering Committee on Nutrition imeundwa ili kusimamia utekelezaji wa azma hiyo.” 


Waziri Mkuu amesema kwamba watu wote wanatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kupambana na matatizo ya lishe nchini, ambapo taarifa za wataalamu zinasema kuwa kwa sasa nchi inakabiliwa na aina mbili za utapiamlo yaani lishe duni na lishe iliyozidi au iliyokithiri. 


Amesema walengwa wakubwa wa lishe duni ni pamoja na watoto chini ya miaka mitano, wanawake walio katika umri wa kuzaa hususani wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na vijana balehe (hususan wa kike). “Hii ni kwa sababu mahitaji ya virutubishi kwa ajili ya miili yao ni makubwa, ukilinganisha na ule unaohitajika na makundi mengine.” 


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post