WAZIRI JAFO AWATAKA MAOFISA ELIMU KUACHA KUWANYANYASA WALIMU

Waziri wa Nchi, Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amewaagiza maofi sa wa elimu wa mikoa na wilaya kuzingatia maadili kwa kuepuka vitendo vya upendeleo na unyanyasaji wa walimu na wanafunzi.


Pia amewataka kujiepusha na suala la uvujishaji mitihani, rushwa na utovu wa maadili. Katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri Joseph Kakunda wakati wa kufungua kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha maofisa elimu wa mikoa na halmashauri kilichofanyika jijini hapa, Jafo alihimiza umuhimu wa kuzingatia maadili na kusisitiza kuwa siku za hivi karibuni, sekta hiyo imejijengea picha mbaya kwa mambo kadhaa.


“Tunatakiwa kuepuka vitendo vya upendeleo na unyanyasaji wa aina yoyote kwa walimu na wanafunzi, uvujaji wa mitihani, rushwa na utovu wa maadili kwa sababu ninyi ni kioo cha jamii,” alisema. 


Jafo alionya kuwa vitendo vya utovu wa maadili kamwe havitavumiliwa na serikali na yeyote anayeendekeza vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali.


“Nitumie fursa hii kulaani vitendo vya unyanyasaji na ukatili vilivyofanywa na baadhi walimu katika Shule ya Msingi Kibeta.”


Aidha, Jafo aliwaasa viongozi hao kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika utoaji wa adhabu kwa wanafunzi kote nchini. 


Alitumia nafasi hiyo kutoa msisitizo kwa viongozi hao kuwajibika kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuitumikia umma, watumishi, wadau na marafiki wa elimu ili kuendeleza imani iliyojengwa kwa umma.


Mkutano huo umewakutanisha watendaji wa elimu katika ngazi ya taifa, mikoa na halmashauri kwa lengo la kukumbushana majukumu, kujipima na kujitafakari utendaji, kupeana uzoefu, kujenga uwezo na kujadiliana juu ya mbinu na mikakati itakayotumika kusaidia kuboresha utoaji wa elimu bora.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post