WATUMISHI TARURA SHINYANGA MBARONI KWA RUSHWA ZA WAKANDARASI


Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Shinyanga inawashikilia watumishi watatu wa wakala wa barabara mjini na vijijini (TARURA) mkoani hapa  kwa tuhuma za kukutwa na fedha za Rushwa walizokuwa wamepewa na wakandarasi kwa ajili ya kuwapitisha kwenye zabuni za ujenzi wa barabara mkoani Shinyanga.

Watumishi hao watatu waliokamatwa kwa tuhuma ya  rushwa ni Njama Kinyemi, Rose Mpuya ambao ni maofisa ugavi TARURA mkoa, pamoja na Matoke Chiyando ambaye ni mhandisi TARURA halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.

Akizungumza na  waandishi wa habari jana, Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono alisema baada ya kupata taarifa juu ya kuwepo kwa rushwa hizo ndipo wakaanza kulifanyia kazi  na hatimaye kufanikiwa kuwakamata watumishi hao wakiwa na fedha za rushwa na kisha kuwasweka rumande kuendelea na uchunguzi zaidi.

“Tumewakata watumishi hao watatu wa TARURA ambao walikuwa kwenye kamati ya kujadili zabuni za ujenzi wa barabara za wilaya zote mkoani Shinyanga, ambapo walikuwa wakiomba rushwa kutoka kwa wakandarasi na baadhi ya fedha wameshawekewa kwenye akaunti zao na zingine zilikuwa kwenye mabegi na mifuko” ,alisema Mkono.

“Watumishi hawa wote watatu tunawashikilia na wapo mbaroni tunaendelea na uchunguzi zaidi na upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani ,”aliongeza.

Kwa upande wake mratibu wa Wakala wa barabara TARURA mkoani Shinyanga Ezekiel Kunyarara alisema yupo safarini, hivyo na kuomba waandishi wa habari wawasiliane na Ofisa utumishi Jafari Mwenda ambaye alikiri kukamatwa kwa watumishi hao, na kubainisha sakata hilo hawezi kulizungumzia zaidi mpaka bosi wake huyo.

Na Marco Maduhu- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527