SERIKALI YASITISHA SH MILIONI 50 KWA KILA KIJIJI


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema wananchi wasitegemee kupelekewa fedha Sh50 milioni walizoahidi mwaka 2015 katika kipindi cha uchaguzi kwa kila kijiji. 

Ameyasema hayo leo Septemba 10, 2018, katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma, kwamba hawatapelekewa fedha hizo na badala yake zitapelekwa kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.


Amesema kuliko kuwapa fedha hizo kwa kila kijiji Serikali imeamua kuwekeza katika elimu, afya, barabara pamoja na maji lengo ni kupeleka maendeleo katika nchi.


"Serikali ya awamu ya tano imeamua kujitegemea katika kujitegemea lazima tujiwekee mikakati kuleta maendeleo katika nchi yetu.”


“Tumeanza kuwekeza katika maswala ya usafiri wa anga na nyie ni mashahidi mmeshuhudia tukinunua ndege zetu," amesema Samia Suluhu


Amesema Serikali imeamua kujitegemea lakini sio kujitegemea asilimia miamoja, kwani wataendelea kuhitaji misaada lakini ni kuna changamoto au vipaumbele vya kitaifa katika vipaumbele hivyo pesa itakayo patikana itashuka hadi kwa mwananchi wa chini.


"Tumeamua kujenga reli itakavyokuwa inaenda haraka na kubeba mizigo mingi zaidi na ikifanya kazi faida yake itafika mpaka kwa wananchi wa chini,” amesema


Amesema Serikali imeamua kuweka umeme mkubwa utakaowaka nchini nzima bila kuzimika ambao utatumika kwenye viwanda vitakavyojengwa Tanzania na faida yake itawafikia wananchi wote.


"Fedha hizo ambazo tumesema tutawapa katika kila kijiji tungeweza (kugawa) kwa kila mtu tusingeweza kuona faida yake.”


“Kwa hiyo sisemi tunaifuta ahadi yetu ipo kwenye ilani ya uchaguzi chama kimetuagiza ni wajibu wetu Serikali kutekeleza, lakini maendeleo kuna kupanga na kuchagua katika mipango yetu ya sasa hivi, hilo tumeliweka pembeni kwanza," amesema makamu huyo.


Amesema wasikae na kudanganya watu kwamba kuna fedha hizo zinatoka serikalini zinakuja zitaingizwa katika miradi muhimu kuliko kuwapa fedha mkononi na ukizingatia serikali inatoa fedha nyingi katika kuhudumia sekta ya elimu. 


Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa mkoa huo, Emmanuel Maganga amesema wananchi wa kijiji hicho ni muhimu kuzingatia afya zao na lishe kwa watoto kwa kuwapa chakula bora.
Na Happiness Tesha, Mwananchi

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527