MUHIMBILI YATENGANISHA WATOTO WALIOUNGANA TUMBO, KIFUA

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanya upasuaji mkubwa wa watoto pacha walioungana sehemu ya tumboni na kufanikiwa kuwatenganisha watoto hao wenye jinsia ya kiume.


Upasuaji huo ambao ulitumia saa tano ulifanywa na wataalamu wa upasuaji wa Muhimbili kwa kushirikiana na watalaamu kutoka Ireland.


Akizungumza na waandishi wa habari jan, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema hospitali imefanikiwa kufanya upasuaji kwa mafanikio na kwamba upasuaji huo umewezekana baada ya kuboreshwa kwa miundombinu ya utoaji huduma katika vyumba vya upasuaji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wataalamu.


Prof. Museru amesema kuongezwa kwa vyumba hivyo kumesaidia kupunguza msongamano wa huduma ya upasuaji na hivyo kurahisisha utoaji huduma kwa watoto kutoka mara 4 hadi mara 10 kwa wiki.


Amesema awali baada ya watoto hao kufikishwa Muhimbili walilazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha.


Naye Daktari Bingwa Upasuaji wa Watoto, Dkt. Petronila Ngiloi amesema walishirikiana vyema na wataalamu wa upasuaji kutoka Ireland katika kuhakikisha watoto hao wanatenganishwa na kwamba lengo kubwa lilikuwa ni kupunguza hatari yoyote inayoweza kutokea kwa watoto hao wakati wa upasuaji.


Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto, Dkt. Zaituni Bokhary amesema upasuaji huo ulihusisha timu ya wataalamu 10 wa upasuaji wa watoto, wauguzi na wataalamu wa tiba ya usingizi.


“Nashauri watoto pacha walioungana au wenye matatizo ya kiafya waletwe Muhimbili ili wafanyiwe uchunguzi wa kina na baada ya kujiridhisha tutawapatia huduma stahiki,” amesema Dkt. Bokhary.
Watoto pacha wakiwa wamelazwa wodini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kabla ya kufanyiwa upasuaji na wataalamu wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ireland.
Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutoka kulia, Dkt. Zaitun Bokhary, Dkt. Petronila Ngiloi na Dkt. Victor Ngotta wakiwafanyia upasuaji wa kuwatenganisha watoto pacha waliokuwa wameungana kwa kushirikiana na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto kutoka Ireland, Prof. Martin Carbally.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu upasuaji wa kuwatenganisha watoto pacha waliokuwa wameungana sehemu ya tumboni. Watoto hao hivi sasa wanaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post