MAJALIWA : SERIKALI HAIJANYANG'ANYA MADARAKA YA TAWALA ZA MITAA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Serikali na Kamati ya Utendaji ya ALAT Taifa, mara baada ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 34 wa ALAT Taifa leo Septemba 27, 2018 unaofanyika jijini Dodoma. Mkutano huo ulioanza Septemba 24, 2018, utamalizika kesho Septemba 28, 2018 kwa kufungwa na Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai. (Picha na Yusuph Mussa).

*****
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haijaondoa Sera ya Ugatuaji Madaraka, bali iliamua kurudisha baadhi ya majukumu ya idara kusimamiwa na wizara badala ya halmashauri kutokana na kushindwa kusimamia vizuri majukumu yake.

Akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) leo Septemba 27, 2018 kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema baadhi ya majukumu hayo kurudishwa wizarani, kumeleta ufanisi mkubwa katika utekelezaji wake.

Majaliwa alitaja idara ambazo majukumu yake yamerudishwa kusimamiwa na wizara moja kwa moja badala ya halmashauri ni zile zilizopo kwenye Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo na Mifuko, na Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

"Licha ya dhana nzuri ya ugatuaji madaraka, Serikali iliamua kurudisha kwenye Wizara Mama baadhi ya majukumu kutokana na udhaifu wa usimamizi ulioonejana chini ya halmashauri. Kwa kufanya hivi hatuna maana ya kupunguza madaraka ama nguvu ya utendaji wa halmashauri, bali ni kuimarisha mfumo wa ugatuaji.

"Sote tunahitaji kufanya shughuli za wananchi ziweze kwenda mbele na miradi yake iweze kuonekana katika utekelezaji. Viongozi wa halmashauri, mameya, wenyeviti na wakurugenzi, ni vema sasa mkasimamia kuona udhaifu huu mnauondoa kwenye halmashauri zenu ili isije ikaonekana kurudisha majukumu kutoka halmashauri kwenda wizarani ndiyo sahihi", alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema, pamoja na idara hizo, pia Serikali Kuu imeona isimamie Hospitali za mikoa na zile za rufaa, huku hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati ndiyo zitakuwa chini ya halmashauri.

Alisema Serikali za Mitaa ndiyo wapo karibu na wananchi, hivyo wataendelea kuziwezesha halmashauri hizo kwa kuzipelekea fedha, lakini madiwani waache kuvutana namna ya kutumia fedha hizo, kwani imebainika kwa baadhi ya halmashauri ambazo zilipewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ama makao makuu ya halmashauri na wilaya, zilileta mvutano na Serikali kutaka kuzirejesha fedha hizo Hazina.

Majaliwa ametoa onyo kwa fedha za mikopo kwa ajili ya wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na walemavu asilimia mbili, kwani zamani halmashauri hizo zilikuwa zinatoa fedha hizo kutoka kwenye mapato yao ya ndani kwa kujisikia, lakini sasa watatoa kisheria, na halmashauri ambayo itashindwa kutoa fedha hizo itashughulikiwa.

Akijibu risala ya Mwenyekiti wa ALAT Taifa Gulam Hafeez Mukadam, Waziri Mkuu, alisema Serikali itafanyia kazi fedha za miradi ya maendeleo zifike kwa wakati, lakini kuongeza posho ya madiwani hali ya kifedha itakaporuhusu. Lakini kwa watumishi, Serikali imekuwa inaongeza watumishi kila mwaka wa fedha ili kukidhi mahitaji.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Suleiman Jafo alisema kwa sasa halmashauri nchini zinapita kwenye mabadiliko makubwa ya kiutendaji tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, na mabadiliko hayo yameleta ufanisi makubwa kiutendaji, kwani uwajibikaji umeongezeka na kumekuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, huku baadhi ya wizi na hujuma vikipungua.

Jafo alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano uliopo kati ya wakurugenzi, wenyeviti na mameya kwenye halmashauri pamoja na usimamizi mzuri wa chombo cha ALAT.

Mwenyekiti wa ALAT Taifa Mukadam alisema moja ya kikwazo katika utendaji ni kuchelewa kama sio kutofika kabisa fedha za miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida, kwani kunazorotesha miradi na shughuli za kila siku za halmashauri.

Mukadam alisema changamoto nyingine ni uhaba wa watumishi na posho za madiwani, kwani bado kiwango wanacholipwa hakikidhi mahitaji yao kutokana majukumu yao kuwa mazito.

Na Yusuph Mussa - Dodoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua  Mkutano Mkuu wa 34 wa ALAT Taifa leo Septemba 27, 2018 unaofanyika jijini Dodoma.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post