Taharuki Shinyanga: ATANGAZIWA MSIBA AKIWA HAI KWA KUFANANISHWA NA ALIYEUAWA KWENYE CHOO CHA SHULE LEO

Taharuki ya aina yake imetokea baada ya Luhaga Mandago (28) ambaye ni mkazi wa Kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga, kukuta nyumbani kwao amewekewa msiba wakati akiwa hai baada ya kufananishwa na marehemu aliyefahamika kwa jina moja la Utumbo aliyeuawa usiku wa kuamkia leo.


Utumbo ambaye hajafahamika makazi yake amekutwa ameuawa usiku wa kuamkia leo Jumatano Septemba 19,2018 katika choo cha shule ya Msingi Jomu mjini Shinyanga kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.


Utumbo aligunduliwa na wapita njia leo majira ya saa moja asubuhi, na kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa huo wa Jomu, ambao nao wakalitaarifu Jeshi la Polisi ambao walifika eneo la tukio na kisha kuondoka na marehemu.


Aidha wakati wananchi walipokuwa wakijaribu kuutambua mwili huo wa marehemu, baadhi yao wakasema wanamfahamu kuwa ni Luhaga Mandago, ndipo walipofuatwa ndugu zake na kisha kuondoka na mwili wake wakiwa na Jeshi la Polisi hadi hospitali ya mkoa wa Shinyanga, kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kisha kuuhifadhi mochwari kwa maandalizi ya mazishi.


Wakati taarifa hizo zikizagaa mitaani kuwa Mandago amefariki na msiba kuanza kuwekwa nyumbani kwao, ndipo jirani yake Yusuf Ahmed akakutana na Mandago na kumweleza juu ya tukio hilo na kumsihi awahi nyumbani ili ndugu na jamaa wakifika wamkute kuwa ni mzima/hajafa, bali amefananishwa tu na marehemu Utumbo.


“Baada ya kukutana na Mandago nikamwambia ndugu yangu sasa hivi wewe ni marehemu, umefananishwa na mtu ambaye ameuawa kwenye choo cha shule ya msingi Jomu, hivyo wahi nyumbani kwenu utakuta umewekewa msiba, ili wanazengo wakuone kuwa ni mzima hujafa,”alisema Ahmed.

Naye Dada wa Mandago, Mary Luhaga alidai kusikitishwa na tukio hilo la mdogo wake kufananishwa na marehemu, ambapo tayari walikuwa wameanza kutaarifiana ndugu na jamaa na marafiki kuwa wamepata msiba, na baada ya kuambiwa kuwa Madango ni mzima wakatengua taarifa za msiba, na kwenda polisi kukanusha kuwa mtu aliyeuawa siyo ndugu yao.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Kamishina msaidizi wa Polisi Simoni Haule, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha Jeshi bado linafanya uchunguzi juu ya mauaji hayo, ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha Maiti katika hospitali ya rufani ya mkoa huo.

Na Marco Maduhu - Malunde1 Blog

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI

Gari la Polisi likiwa limebeba mwili wa marehemu ambaye alifahamika kwa jina moja la Utumbo, aliyeuawa katika choo cha Shule ya Msingi Jomu manispaa ya Shinyanga, ambapo hapo awali mwili huo ulifananishwa na Luhaga Mandago mkazi wa Kata ya Kambarage, ambapo ndani ya gari hilo la Polisi pia wapo ndugu zake na Mandago mara baada ya kupewa taarifa ndugu yao amekufa, lakini baadae wakapewa taarifa kuwa Mandago ni mzima yupo nyumbani na hatimaye kutengua taarifa za msiba huo.Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 Blog

Jeshi la Polisi likiondoka na mwili wa marehemu kwenda kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya uchunguzi na kuuhifadhi mochwari.

Wananchi wa mjini Shinyanga wakishuhudia tukio hilo la Mauji katika choo cha Shule ya msingi Jomu manispaa ya Shinyanga.

Damu ya marehemu ikionekana eneo la tukio mahali ambapo yamefanyika mauaji.

Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post