LOWASSA ; SITISHWI NA WABUNGE 16 WA CCM WALIOKUJA KUPAMBANA NAMI

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa amesema wabunge 16 wa CCM waliopo Monduli katika kampeni za uchaguzi wa ubunge za chama hicho tawala hawamtishi.

Lowassa ametoa kauli hiyo jana Septemba 4, 2018 katika kata ya Meserani kwenye kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Yonas Laiser.

Amesema CCM wamewapeleka Monduli wabunge 16 kupambana naye, “lakini wanatakiwa kuangushwa kwa wananchi kumchagua mgombea wa Chadema.”

Lowassa aliyeongoza jimbo hilo kuanza 1995 hadi 2015, ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku kadhaa baada ya CCM kupeleka wabunge wake hao kuhakikisha mgombea wa chama hicho, Julius Kalanga anaibuka na ushindi.

Katika mkutano huo wa kampeni, Lowassa aliwataka wakazi wa Monduli kuwaaibisha CCM kwa kumchagua Laiser kwani ana uwezo wa kuwasaidia.

Amesema Chadema walimuamini Kalanga na kumsaidia kuwa mbunge mwaka 2015 lakini amewasaliti wananchi.

"Kalanga tulimleta hapa mkamchagua ametusaliti sasa muonyesheni adhabu msimchague tena," alisema.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema amewataka wakazi wa Monduli kumchagua Laiser ili kulinda hadhi na heshima ya Lowassa.

Lema amesema uchaguzi wa Monduli unafanyika baada ya Kalanga kujiunga CCM akitokea Chadema, ili kummaliza nguvu Lowassa.

"CCM wanataka kutumia uchaguzi huu kumdhoofisha Lowassa kuelekea uchaguzi wa 2020 hivyo wananchi Monduli msikubali Lowassa kudhoofishwa huyu ni kiongozi wenu wa mila," alisema.

Kwa upande wake, Laiser aliomba achaguliwe na hatawasaliti.

Laiser ambaye ni diwani wa Chadema kata ya Lepurko amesema ana uwezo wa kutatua kero za wananchi wa Monduli kwani anazijua.

"Najua kuna shida ya maji, migogoro ya ardhi nichagueni tutashirikiana kuzitatua," amesema.

Chanzo-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527