RAIS MAGUFULI AAGIZA KUJENGWA KWA KIVUKO KIPYA UKEREWE...AMTAKA WAZIRI ATANGAZE ZABUNI HARAKA


Kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Septemba 20, 2018.

Rais John Pombe Magufuli amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Isaack Kamwele kuitisha mapema iwezekanavyo zabuni ya ujenzi wa kivuko kipya ili wananchi wa Bugolora na Ukara wapate huduma nzuri baada ya kile cha MV Nyerere kuzama.

Hilo limebainishwa leo na Waziri mkuu Kassim Majaliwa, wakati akiongea kwenye eneo la tukio huko Ukara, Ukerewe, ambapo amesema pamoja na maamuzi ya kuvunja bodi ya TEMESA na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya SUMATRA, lakini pia Rais Magufuli ameagiza ujenzi wa kivuko kipya, kitakachohudumia wakazi wa eneo la Ukara na Bugolora.

''Rais ameagiza leo Waziri aitishe zabuni ya ujenzi wa kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba tani 50, na abiria zaidi ya 200 na itakuwa na uwezo mara mbili ya Mv Nyerere pia kiwe na uwezo wa kufanya safari nyingi ili kuepusha kuzidisha watu'', amesema.

Pia Waziri mkuu amemsisitiza waziri Kamwele ikiwezekana kufikia kesho awe ameshatangaza zabuni hiyo na ujenzi uanze mara moja ili wananchi wapate huduma ya haraka.

Aidha Waziri Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo, kuhakikisha kivuko cha Mv Nyerere kinaondolewa majini vizuri na kisivutwe ili kuepusha uharibifu na hatimaye kiweze kuchunguzwa na kama kitawezekana kufanyiwa marekebisho kifanyiwe na kikikamilika kisaidiane na kivuko kipya.

Kivuko cha Mv Nyerere ambacho kilizama Alhamis ya Septemba 20, 2018, kilikuwa na uwezo wa kubeba tani 25 pamoja na abiria 100. Katika ajali hiyo imebainika kivuko hicho kilizidisha idadi ya watu pamoja na mizigo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post