MGODI WA DHAHABU WA BULYANHULU WALIPA MILIONI 59 KWA AJILI YA USHURU WA HUDUMA KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA NYANG’HWALE

Kampuni ya Acacia, kupitia Mgodi wake wa Dhahabu wa Bulyanhulu umekabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 59,769,145.90/- kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale kwa ajili ya malipo stahiki ya ushuru wa huduma wa kipindi cha miezi sita ya mwanzoni mwa mwaka 2018, fedha ambazo zitasaidia uboreshaji wa huduma za jamii wilayani humo.

Hundi hiyo imekabidhiwa leo kwa uongozi wa Halmashauri hiyo na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Bwana Benedict Busunzu katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale.

Akikabidhi hundi hiyo, Busunzu amesema jumla ya ushuru wa huduma wa Mgodi wa Dhahabu Bulyanhulu katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka 2018 ni shilingi milioni 181,118,623, hivyo Halmashauri ya Nyang’hwale imelipwa asilimia 33 ya ushuru huo na kwamba asilimia 67 ya ushuru huo yenye thamani ya shilingi milioni 121,349,478/- yamelipwa katika Halmashauri ya Msalala kwa mujibu wa makubaliano kati ya Mgodi na Halmashauri hizo mbili.

Amebainisha kuwa kila baada ya miezi sita Mgodi hulipa ushuru huo kwa mujibu wa sheria, ambapo fedha hizo ni asilimia 0.3 ya ukokotoaji wa ushuru wa huduma ya mgodi huo kwa kila kipindi cha miezi sita.

“Makubaliano yetu na Halmashauri ya Msalala na Nyang’hwale ni kuhakikisha fedha hizo zinatumika kuboresha huduma za jamii katika sekta mbalimbali kama vile elimu, afya, miundombinu na maji.”

Wakipokea hundi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Hamim Gwiyama na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale Mariam Chaurembo wamesema watahakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwenye miradi ya jamii iliyo ya kipaumbele kwa ajili ya kuboreshea wananchi wa wilaya hiyo huduma za kijamii kama elimu, afya na huduma jumuishi za jamii.

“Ni kweli kwamba mapato kwa wilaya yetu yanayotokana na ushuru wa huduma kwa wilaya yetu yameshuka lakini tunaamini kwamba mara mgodi utakapoanza tena uzalishaji wake mapato yataongezeka hivyo kwa sasa kinachotakiwa ni ubunifu wa vyanzo vingine kwani wilaya yetu ina vyanzo vingine vya mapato kikubwa ni ubunifu wa kuhakikisha vyanzo hivyo vinaleta tija. 

Pia nawaonya watendaji wote wa halmashauri hii wasithubutu kutumia vibay fedha za umma kwa sababu hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kama ambavyo tayari watuhumiwa saba tumewakamata na wawili tumewafukuza kazi kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma wilayani humu, alisema Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Hamim Gwiyama

“Mpaka sasa fedha hizo za ushuru wa huduma kutoka Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu tumeshazipokea na tayari tumeshazipangia namna tutakavyozitumia kwa ajili ya miradi mbalimbali ya uboreshaji wa huduma za jamii, hakuna pesa itakayotumika vibaya katika uongozi wetu kwani tumeshajipanga na tunafuatilia kwa karibu sana idara husika zinazopangiwa kutumia fedha hizo, hatuko tayari kuona tukio la ubadhirifu wa fedha katika wilaya yetu linajitokeza tena".

Mapema mwezi huu Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu umesaini hati ya makubaliano kutoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuchangia vifaa vya umaliziaji wa ujenzi wa zahanati 32 za vijiji wilayani Nyang’hwale katika juhudi za kampeni ya kijiji kimoja zahanati moja.

 Pia mwezi Machi mwaka huu mgodi wa Bulyanhulu na wa Buzwagi kwa pamoja ilichangia vifaa yvya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 150 kwa halmashauri ya Msalala na Halmashauri ya Wilaya ya Kahama Mji kusaidia juhudi za ujenzi wa mamia ya madarasa katika shule za sekondari na msingi.

Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na migodi mingine ya Acacia nchini hulipa ushuru wa huduma kwa wilaya husika kila baada ya miezi sita. Tangu mwaka 2000 hadi 2017 Mgodi wa Bulyanhulu Umeshalipa zaidi ya shilingi Bilioni 9 kwa halmashauri za Msalala na Nyang’hwale.
Wa pili kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Bwana Benedict Busunzu akishikana mkono na mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Hamim Gwiyama wakati wa kukabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 59,769,145.90/- kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Makabidhiano yakiendelea
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Bwana Benedict Busunzu akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ya hundi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Hamim Gwiyama akizungumza wakati wa makabidhiano hayo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale Mariam Chaurembo akizungumza wakati wa makabidhiano hayo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post