HAJI MANARA ABARIKI KAIMU RAIS WA SIMBA 'TRY AGAIN' KUNG'OKA


Afisa habari wa Simba, Haji Manara

Afisa habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amebariki uamuzi wa Kaimu Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah maarufu ‘Try Again’ kutochukua fomu ya kugombea uongozi ndani ya klabu hiyo katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Novemba.

Manara amesema kuwa kiongozi huyo ameamua kutochukua fomu ya kugombea licha ya kuombwa na viongozi mbalimbali wa mpira na serikali.

“Ameamua kutogombea kwa hiari yake ingawa kulikuwa na maombi mengi kutoka kwa viongozi mbalimbali wa mpira na serikali, lakini yeye anaamini amesimamia vizuri mchakato wa mabadiliko ya katiba kwahiyo anaona ni bora awapishe wengine wakaichukua klabu na kuiendeleza”.

Aidha, Manara ameongeza kuwa kwa upande wao kama klabu watatoa tamko rasmi hivi karibuni kuwajulisha wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuhusu kutokuwepo kwa kiongozi huyo katika klabu.

Simba inatarajia kufanya uchaguzi wake 3, Novemba mwaka huu ambapo zoezi la uchukuaji fomu limeshakamilika, jumla ya fomu 21 zikiwa zimeshachukuliwa, fomu mbili kati ya hizo ni za kuwania uenyekiti wa klabu hiyo na zilizobaki ni za kuwania ujumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo.

Waliochukua fomu za kuwania uenyekiti wa klabu hiyo ni, Swedi Khamis Nkwabi na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Mtemi Ramadhani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post