DC AMSWEKA NDANI SAA 48 WAKILI WA KUJITEGEMEA


Wakili wa kujitegemea wa mjini Moshi, Patricia Eric juzi alijikuta katika 18 za mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya baada ya kuswekwa mahabusu ya polisi kwa saa 48.

Hadi jana saa 12:00 jioni, wakili huyo alikuwa akishikiliwa katika kituo cha polisi cha Bomang’ombe mjini Hai, huku mawakili wa kujitegemea wakipiga kambi kujaribu kumtetea.

 Ole Sabaya alipotafutwa jana, alikiri kukamatwa kwa wakili huyo, lakini akasema uamuzi wa kumkamata ni wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kutokana na kufanya makosa ya jinai.

 “Vyombo vinavyohusika vitaendelea naye kisheria huko mahakamani,” alisema Ole Sabaya bila kufafanua makosa ya jinai yanayomkabili wakili huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alipotafutwa jana alisema yuko wilayani Hai na atalizungumzia atakaporejea Moshi, lakini hadi saa 12:00 jioni alikuwa hajarejea ofisini kwake.

Taarifa za kukamatwa kwa wakili huyo, zilianza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii jana, zikieleza kuwa wakili huyo ambaye ni mtoto wa wakili, Eric Ng’maryo alikamatwa juzi.

 Umoja wa watetezi wa haki za binadamu ndio waliokuwa wa kwanza kusambaza taarifa hiyo katika mitandao ya kijamii ikiwamo wa WhatsApp.

Taarifa hiyo ilidai wakili huyo alikamatwa kwa amri ya Ole Sabaya ikiwa ni siku chache baada ya kumuandikia barua mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira akimlalamikia Ole Sabaya.

Mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS) tawi la Kilimanjaro, David Shilatu aliliambia Mwananchi kuwa hadi jana saa 12:00 jioni walikuwa wilayani Hai kufuatilia dhamana ya wakili huyo.

 “Tunaomba ieleweke tu kuwa wakili sio dhambi na wala sio kweli kuwa ni kazi ya kusaidia uhalifu. Tatizo ni mgogoro wa wamiliki wa mashamba wilaya ya Hai na Halmashauri ya wilaya juu ya kodi.Wakili alikuwa akimwakilisha mmoja wa wateja wake ambao ni wamiliki wa mashamba,”alidai.


Septemba 5, 2018, wakili Patricia alimwandikia barua RC Mghwira akilalamikia kile alichodai matumizi mabaya ya ofisi na kuwabugudhi wawekezaji, alikodai kunafanywa na Ole Sabaya.


Wakili huyo alitolea mfano wa wateja wake aliowataja kuwa ni N.G Emmanuels Company Limited na African Vegetables Company Limited, ambao waliitwa kwa simu na mkuu huyo wa wilaya.
Na Daniel Mjema,Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post