MAREKANI YAONESHA WASIWASI UCHAGUZI WA MARUDIO TANZANIA

Marekani imeonyesha wasiwasi wake kuhusu uchaguzi mdogo uliofanyika mnamo tarehe 12 mwezi Agosti nchini Tanzania.

Taarifa iliotolewa na ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam inasema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia na makosa, ikiwemo visa ambapo tume ya uchaguzi nchini humo ilikataa kusajili wagombea wa upinzani.

Ubalozi huo pia ulikuwa na wasiwasi kuhusu vitisho vilivyofanywa na maafisa wa polisi dhidi ya wanachama wa upinzani, kukamatwa kiholela, na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

''Maswala hayo yanahujumu haki ambayo katiba ya Tanzania inawapatia raia wake na kuhatarisha amani na utulivu nchini na katika eneo zima'', ilisema taarifa hiyo.

Mnamo tarehe 12 mwezi Agosti Tanzania ilifanya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Buyungu, jimbo la Kigoma na wadi 36 nchini humo.

Uchaguzi wa Buyungu ulifanyika ili kujaza kiti cha marehemu Kasuku Bilago kutoka chama cha Chadema aliyefariki mnamo mwezi Mei mwaka huu.

Mgombea wa Chama cha mapinduzi CCM Christopher Chiza, ambaye ni waziri wa zamani alitangazwa mshindi wa eneo bunge hilo na tume ya uchaguzi nchini humo NEC.

Kulingana na NEC, bwana Chiza alijipatia kura 24,578 na kumshinda mgombea wa Chadema Elia Fredrick Michael aliyejipatia jumla ya kura 7,668. Fredrick alijipatia kura 16,910.

Katika wadi zote 36 ambapo uchaguzi huo ulifanyika madiwani wa chama cha CCM walitangazwa washindi wa wadi hizo.

Viti hivyo vilikuwa wazi baada ya baadhi ya madiwani kujiuzulu kutoka upinzani na kujiunga na chama tawala CCM, vifo mbali na wale waliopoteza uanachama wa vyama vyao kwa sababu zisizojulikana.

 Soma zaidi <<HAPA>>

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527