
Rais Dkt. John Magufuli amemtuma Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Kikwete kumwakilisha katika sherehe za uapisho wa Rais mteule wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa zitakazofanyika kesho mjini Harare.
Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa asubuhi ya leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Chato Geita na kusema kwamba Dkt, Kikwete atafuatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Bara), Philip Japhet Mangula pamoja na Mwenyekiti wa chama cha UDP, John Cheyo.
Mnangagwa ataapishwa kesho kuongoza nchi ya Zimbabwe baada ya kushinda katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Julai 30 akiwa amepokea kijiti kutoka kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe.
Emmerson Mnangagwa alitangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe kuwa mshindi wa kiti cha Urais kwa kupata jumla ya kura milioni 2.5 sawa na asilimia 50.8 katika uchaguzi huo ambapo mpinzani wake wa karibu, Nelson Chamisa wa Chama cha MDC amepata jumla ya kura milioni 2.15 sawa na asilimia 44.3 ya kura zote alizopigiwa na wananchi wa Zimbabwe.
Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza tangu kiongozi wa muda mrefu wa nchi ya Zimbabwe, Robert Mugabe kung'olewa madarakani na kupelekea kuibua hisia kali za kisiasa nchini humo kwa kile kilichoonekana watu kuchoshwa na tawala za mabavu.
Social Plugin