RAIS MAGUFULI AMPONGEZA MNANGAGWA KWA KUCHAGULIWA KUWA RAIS WA ZIMBABWE

 Rais John Magufuli amempongeza rais mteule wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa kwa kuchaguliwa kuliongoza Taifa hilo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika takribani siku nne zilizopita.

Mnangagwa ameshinda uchaguzi huo baada ya kujikusanyia asilimia 50.8 ya kura huku Nelson Chamisa wa Muungano wa chama kikuu cha upinzani (MDC) akipata asilimia 44.3.

Katika ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Magufuli amesema ushindi huo ni dalili ya imani ya watu wa Zimbabwe kwake.

“Kwa niaba ya Serikali na Tanzania nakutumia salamu za pongezi kwa ushindi wako katika nafasi ya urais. Ushindi wako unaonyesha imani iliyopo kwa watu wa Zimbabwe katika kuwaongoza kwenye mafanikio,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, MDC  umeyakataa matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi Mnangagwa wa chama tawala cha Zanu PF.

Hata kabla ya Tume ya Uchaguzi Zimbabwe kuthibitisha matokeo, maofisa waandamizi wa MDC Morgan Komichi na Nkululeko Sibanda ambaye ni msemaji wa Chamisa waliingia kwenye ukumbi wa kutangazia matokeo na kuyakataa.

Komichi amesema matokeo yanayotangazwa ni ulaghai mkubwa akiongeza hawakutia saini kabla ya kukamatwa na polisi na kutolewa nje.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527