Saturday, August 25, 2018

NACTE YATOA UFAFANUZI KUHUSU MAOMBI YA NAMBA YA UHAKIKI WA TUZO (AVN) KWA WAHITIMU WANAOTAKA KUJIUNGA NA ELIMU YA JUU

  Malunde       Saturday, August 25, 2018
Baraza la Elimu ya Ufundi (Nacte) limebainisha kuwa hakuna mwombaji atakayefanyiwa udahili wa kujiunga a na chuo kama hana namba ya uhakiki wa tuzo (AVN).

Utoaji wa AVN ulianza mwaka jana baada ya kutoka katika mfumo wa udahili wa pamoja kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambapo sasa waombaji wanawasilisha maombi katika vyuo husika.

Akizungumza jana Ijumaa Agosti 24, 2018 juu ya umuhimu wa kuwa na AVN, mkuu wa kitengo cha udahili wa Nacte, Twaha Twaha amesema kabla ya kuwapo kwa mfumo huo, vyuo vilikuwa vinapata tabu kufanya uchaguzi wa wanafunzi wenye sifa za kozi husika.

Amebainisha kuwa walikuwa wanashindwa kujua kama vyeti vya mwombaji husika vya stashahada kama vinatambuliwa na Nacte.

Amefafanua kuwa kabla ya kuwapo kwa AVN hatua ya udahili wa wanafunzi kwenye vyuo ilikuwa ngumu na kusababisha usumbufu mkubwa.

“AVN itaondoa urasimu, ucheleweshaji wa taarifa za mwanafunzi na udanganyifu wa vyeti uliokuwa ukifanyika, ”amesema.

“Kwa kupata AVN chuo kikiingiza katika mifumo yake kinaweza kuona kama ni matokeo, kozi ya mwombaji na taarifa zake nyingine kwa sababu imeunganishwa na vyuo, TCU, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na mifumo mingine ya elimu.”

Amesema kuwa tofauti na hapo wangekuwa wanapata barua nyingi za kuomba uhakiki wa vyeti vya wanafunzi wanaotaka kujiunga na elimu ya juu.

“Kwa mfano mwaka huu 2018 tumeshatoa AVN zaidi ya 9,000 na Nacte inavitambua vyuo 535 ambavyo vimesajiliwa, hivyo unaweza kuona wote hawa wangeleta barua za kuomba uhakiki,” amesema.

Ameeleza kuwa Nacte inaufahamisha umma na wananchi kwa ujumla kuwa huduma ya kuomba na kupewa AVN inafanyika mwaka mzima, hivyo kila anayetaka kujiunga na elimu ya juu lazima awe nayo.

Ameitaja changamoto kubwa wanayokutana nayo kwa waombaji wa AVN ni waombaji kutokamilisha taarifa zao.

Amesema maombi ya AVN hufanyika kwa njia ya mtandao kupitia kwenye tovuti ya baraza.

“Mwombaji hulazimika kuweka taarifa za msingi kadri zinavyotakiwa na mfumo ikiwamo namba ya usajili ya mtihani wa kidato cha nne, mwaka aliohitimu na chuo alichosoma stashahada,” amesema.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post