MZEE MAJUTO AZIKWA SHAMBANI KWAKE TANGA


Mwili wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini, Amri Athumani ‘King Majuto’ umezikwa leo shambani kwake Kiruku,Tanga, ambapo viongozi wa serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, wameshiriki maziko.

Safari ya kwenda Tanga kwaajili ya mazishi ilianza jana saa 10.15 jioni baada ya kumuaga katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, na uliwasili Donge nyumbani kwake 7.05 usiku baada ya kusimamishwa katika vijiji 14 na mashabiki wakitaka kutoa heshima ya mwisho.

Leo kuanzia saa 5.45 mchana, ibada ya mazishi imefanyika katika msikiti wa Nuruguda uliopo karibu na nyumbani kwake na kuzikwa kijiji cha Kiruku yalipo mashamba yake nje kidogo cha jiji la Tanga.

Mwili ulipowasili nyumbani kwa Mzee Majuto, kuliibuka vilio huku wanawake wengi wakizimia, kwa zaidi ya mwaka mmoja jina la Mzee Majuto lilitawala vyombo vya habari likihusishwa na ugonjwa wa henia na baadaye tezi dume.

Januari mwaka huu, Mzee majuto alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam hata hivyo, kidonda cha upasuaji wa henia kiliendelea kumsumbua na alilazwa kwa mara nyingine katika hospitali hiyo katikati ya mwezi Aprili.

Mei 4, mwaka huu Mzee Majuto alisafirishwa kwenda India kupata matibabu katika hospitali ya Apollo, katika Jiji la New Delhi na June 23, mwaka huu Mzee Majuto alirejea nchini baada ya kupata matibabu yaliyokuwa yakigharamiwa na serikali na moja kwa moja alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwaajili ya uangalizi kabla ya kuruhusiwa na kisha kurudishwa tena Julai 31 hospitalini hapo.

Hali ya mzee Majuto ilianza kubadilika siku ya tarehe 8, Agosti majira ya saa tisa alasiri ambapo alitolewa kutoka jengo la sewahaji na kuhamishiwa chumba cha uangalizi maalum (ICU), na ilipofika mida ya saa 2:00 usiku alifariki Dunia katika hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar esa salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527