WALIOMUUA BILIONEA MSUYA WAGOMA KUNYONGWA


Watu watano waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua kwa makusudi mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, Erasto Msuya, wamewasilisha notisi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga adhabu hiyo.


Hukumu dhidi ya washtakiwa hao watano ilitolewa Julai 23 na Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu, ambapo pia alimwachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne au Mredii.


Waliohukumiwa kunyongwa ni mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed; wa tatu, Mussa Mangu; mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa; wa sita Sadik Jabir na wa saba, Ally Majeshi.


Ingawa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Frank Mahimbari hakupatikana jana kuelezea suala hilo, lakini Wakili Hudson Ndusyepo aliyekuwa akimtetea Sharifu alithibitisha suala hilo. Hata hivyo, wakili huyo alitaka atafutwe Wakili Majura Magafu au John Lundu ambao walikuwa miongoni mwa mawakili wa utetezi, akisema wao ndio walioandaa notisi ya kukata rufaa.


Akizungumza na gazeti hili jana, Magafu aliyekuwa miongoni mwa waliounda jopo la mawakili wanne wa utetezi, alisema tayari wamewasilisha notisi hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania.


“Ni kweli tumetoa notice of appeal (ilani ya kukata rufaa). Kinachofuata ni Mahakama Kuu kuandaa kumbukumbu za shauri hilo na wakishaziandaa wanazipeleka Mahakama ya Rufani,” alisema.


Kwa mujibu wa wakili huyo anayetokea jijini Dar es Salaam, baada ya Mahakama Kuu kuandaa nyaraka hizo na kuzipeleka Mahakama ya Rufani, watawapa nakala wao ili waweze kuandaa sababu za rufaa.


Ukataji rufaa


Akizungumzia utaratibu wa kukata rufaa, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) mkoani Kilimanjaro, Wakili David Shillatu alisema rufaa za aina hizo za jinai husikilizwa na majaji watatu.


“Sasa hivi bado ni hatua za awali baada ya kupokea hizo kumbukumbu, wanaandaa sababu za rufaa na kuziwasilisha Mahakama ya Rufani na baadaye majaji watatu hukaa kuisikiliza,” alisema Shillatu.


“Wakishasikiliza wanaweza kuja na hukumu mojawapo kati ya hizi. Ama ku-upheld (kuhuisha) hukumu na adhabu au kutupilia mbali rufaa au kuagiza kusikilizwa upya kwa kesi.”


Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita ya sub machine gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.


Katika eneo la tukio kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22, huku gari lake aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola na simu zake mbili zikikutwa eneo la tukio.


Hukumu ilivyokuwa


Akitoa hukumu ya adhabu ya kifo, Jaji Maghimbi alisema mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo ya washtakiwa wanne na pia ushahidi huru kuunga mkono.


Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokewa mahakamani na kusomwa, yalieleza mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa kila mmoja ni ya Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Majeshi.


Kwa mujibu wa jaji huyo, maelezo ya Sharifu ambayo yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri yanaeleza mpango wa mauaji ulivyosukwa na bunduki ya SMG ilivyonunuliwa.


Pia katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo alieleza namna laini mpya za simu zilivyosajiliwa kwa majina ya Kimasai na pikipiki mbili zilizotumika katika mauaji hayo zilivyonunuliwa.


Kuhusu mshtakiwa wa tatu, Jaji Maghimbi alisema ingawa katika maelezo yake ya kukiri kosa alianza kwa kujitoa na kuwabebesha mzigo washtakiwa wenzake, lakini alishiriki katika nia hiyo ovu.


“Ingawa alianza maelezo hayo ya kukiri kosa kwa kujitoa lakini alijua mpango huo wa mauaji na akaendelea kushiriki katika mipango hiyo ya mauaji hadi mwisho bila kujitoa,” alisema Jaji Maghimbi.


“Kitendo cha kutojitoa katika mpango mzima wa mauaji inaonyesha nia yake ovu ya kutenda kosa hilo. Hakufanya juhudi zozote za kujitoa katika mipango hiyo miovu ya mauaji,” alisisitiza jaji.


Jaji Maghimbi alisema maelezo ya mshtakiwa Karim anayeeleza kuwa ndiye aliyemfyatulia risasi nyingi Msuya, hadithi yake inaunganika na yale waliyoeleza Sharifu, Mussa na Majeshi.


Jaji alisema maelezo hayo ya kukiri kosa na maungamo ya washtakiwa, yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri na hivyo kuthibitisha shtaka la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.
Na Daniel Mjema, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527