MLINZI KAMPUNI YA LAKE SECURITY AUAWA KWA KUPIGWA RISASI MWANZA


Mlinzi wa kampuni ya Lake Security, ameuawa kwa kupigwa risasi tumboni na mlinzi mwenzake baada ya kuzuka ugomvi kati yao wa kudaiana Sh. 30,000.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alimtaja aliyeuawa kwa risasi kuwa ni Charles Pendo (24) mkazi wa Bukokwa, wilayani Sengerema.

Alisema Pendo aliuawa saa tatu juzi usiku akiwa kwenye lindo baada ya kupigwa risasi tumboni na kutokea mgongoni.

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, Pendo aliuawa na mlinzi ambaye ni mfanyakazi mwenzake wa Lake Security, Octavian Wilson (35) mkazi wa Mabatini, jijini Mwanza kwa bunduki aina ya Rifle yenye namba TZCAR 80856.


Alisema Pendo alifariki dunia papo hapo na mtuhumiwa wa mauaji hayo alitorokea kusikojulikana.


Kamanda Msangi alisema chanzo cha mauaji hayo ni deni la muda mrefu la Sh. 30,000 ambalo Wilson alikuwa akidaiwa na Pendo.


Inadaiwa kuwa baada ya walinzi hao kuingia kazini lindoni, Pendo alimfuata mtuhumiwa na kumweleza kuwa anaomba amlipe fedha zake lakini mtuhumiwa alikaidi na kusababisha kuzuka ugomvi kati yao.


"Mlinzi mwenzao alifika na kuwasuluhisha ndipo walimwachia mtuhumiwa silaha zote na wao (Pendo na msuluhishi) kwenda kukagua milango ya maduka waliyokuwa wakilinda. Baada ya kumaliza ukaguzi huo, wawili hao walirudi mahali alipokua amekaa mtuhumiwa ndipo ghafla mtuhumiwa alisimama na kumfyatulia Pendo risasi iliyolenga maeneo ya tumbo na kutokea mgongoni.


“Kitendo hicho kilisababisha Pendo kupoteza maisha huku mtuhumiwa alitoroka eneo la tukio akiwa na silaha zote mbili, yake na ile ya marehemu," alisema Msangi.


Alisema wananchi walitoa taarifa polisi na askari walifika eneo la tukio na kuanza kufanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na wananchi na baadaye walifanikiwa kukamata silaha hizo mbili zenye namba TZCAR 80856 aina ya Riffle na TZCAR 41445 aina ya Short gun ambazo mtuhumiwa alizitelekeza.


Kamanda Msangi alisema, mpaka jana mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa hajakamatwa, huku msako mkali wa kumtafuta katika maeneo mbalimbali ukiendelea.


"Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya uchunguzi, pindi utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi," alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post