Sunday, August 19, 2018

MISA - TAN YALAANI WAANDISHI WA HABARI KUPIGWA

  Malunde       Sunday, August 19, 2018

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan) imesikitishwa na vitendo vya askari wa Jeshi la Polisi kuwapiga waandishi wa habari wakiwa wanatekeleza majukumu yao.Imesema kitendo hicho ni ukiukwaji wa tamko la haki za binadamu huku wakilitaka jeshi la polisi kuomba radhi kwa vitendo hivyo na kuwachukulia hatua askari waliohusika.


Hayo yamesemwa leo Jumapili na Mwenyekiti wa Misa-Tan, Salome Kitomary akizungumzia matukio mawili ya waandishi wa habari, Sillas Mbise wa Wapo Redio na Sitta Tuma wa gazeti la Tanzania Daima waliopigwa na polisi wakitekeleza wajibu wao.


Kitomary amesema waandishi wa habari wanafanya kazi ili kuhakikisha kuwa haki hiyo inakuwepo ili kujenga demokrasia na kulinda utawala wa sheria.


“MISA Tanzania, inasikitishwa na vitendo vya hivi karibuni vya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji kwa waandishi wa habari unaoendelea nchini wakati wakitekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma,” amesema Kitomary


"Tunaungana na wadau wote wa habari na watetezi wa haki za binadamu kupinga vikali vitendo vya kiudhalilishaji kwa mwandishi wa habari za michezo wa Wapo Radio, Sillas Mbisse kwa kupigwa na polisi akiwa chini ya ulinzi wa polisi hao wakati akitekeleza wajibu wake wa kukusanya habari katika Uwanja wa Taifa, Agosti 8 mwaka huu jijini Dar es salaam," ameongeza


Amesema tukio hilo la kufedhehesha na kusikitisha lilitokea siku ya mpambano kati ya Simba na Asante Kotoko ya nchini Ghana katika siku ya Simba ‘Simba Day.’


"Michezo huwakusanya watu pamoja bila kujali rangi zao, itikadi, historia, dini, imani na hadhi ya mtu. Ni maajabu sana kwa mwanahabari kupigwa na polisi mbele ya watu na si mashabiki wa timu bali na watu wenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao," amesema Kitomary.


Amesema Misa-Tan inaungana na wadau wengine kupinga kitendo cha kupigwa na kunyanyaswa kwa mwandishi wa habari Sitta Tuma katika kata ya Turwa wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.


Kitomary amesema Tuma ni mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima alikamatwa na kisha kupigwa na polisi wakati akikusanya habari za uchaguzi na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi wilayani humo.


“Vitendo hivi si tu kwamba vinaondoa uhusiano mzuri wa utendaji kazi kati ya polisi na wanahabari lakini pia vinawanyima haki wanahabari kukusanya habari na raia kupewa taarifa iliyokamilika,” amesema.


“Misa-Tan inapinga vikali vitendo hivi viovu na ukandamizwaji wa wanahabari na haki za kupata habari na kuwaomba wenye mamlaka kuomba radhi na kisha kuchukua hatua stahili kwa waliotenda vitendo hivi vinavyochafua jeshi la polisi nchini.”


Katika kusisitiza hilo, Misa-Tan itaendelea kupinga unyanyaswaji dhidi ya waandishi wa habari, watetezi wa haki za binaadamu, wanaharakati kupitia mitandao ya kijamii na kuitaka mamlaka husika kuendeleza haki za binaadamu kwa kuzingatia viwango katika vyombo vya habari kuwa huru.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post