Saturday, August 11, 2018

MCT & TASWA : UKATILI DHIDI YA WAANDISHI WA HABARI HAUTAFUMBIWA MACHO

  Malunde       Saturday, August 11, 2018
Katibu Mtendaji wa MCT Kajubi Mukajanga
 
Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) wamesema matukio ya kikatili wanayofanyiwa wanahabari wakiwa kazini hayatafumbiwa macho kwani si udhalilishaji wa taaluma pekee bali pia ni hujuma kwa tasnia.


Tamko la taasisi hizo limekuja kufuatia tukio la polisi kumshambulia mwandishi wa habari wa kituo cha Wapo Radio cha Dar es Salaam, Silas Mbise Jumatano Agosti 8, 2018 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.


Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha Mbise akishambuliwa na askari zaidi ya mmoja huku akiwa amevuliwa shati.


Kwa mujibu wa tamko hilo kitendo hicho kina nia ya kudhoofisha uhuru wa kupatikana kwa habari na usambazaji wa habari kwa jamii ikiwa ni nguzo kuu kwenye mfumo wa kidemokrasia, ambao tunajitahidi kuuimarisha nchini.


Tamko hilo lililosainiwa na Katibu Mtendaji wa MCT Kajubi Mukajanga na Katibu Mkuu wa Taswa, Amir Muhando limeeleza kuwa kitendo hicho ni kinyume na ibara ya 13(6) (e) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokataza mtu kuteswa.


‘Hivyo basi, kukaa kimya, hata tukiliwazwa na kuombwa samahani kwa jambo hili, hakutatoa tafsiri nyingine kwa wana taaluma. Tunatarajia jeshi la polisi kufanyakazi zake kwa kufuata sheria na weledi wa kazi na kuwa walinzi wa amani na mali za wananchi,” limesema.


“Mbise kwa sasa yupo katika matibabu kutokana na kipigo hicho. Tunataka polisi wote waliohusika katika kitendo hiki cha kikatili wachukuliwe hatua kali ili wasiendelee kulipa taswira mbaya jeshi zima la polisi.”


Taasisi hizo pia zimewataka wadau wa michezo ikiwa ni pamoja na polisi, wachezaji, viongozi ana mashabiki mwenye malalamiko kwa mwandishi wa habari binafsi, au chombo chake afuate taratibu za kistaarabu zilizopo, ikiwemo kuwasiliana na uongozi wa chombo cha habari husika na wakishindwa kuafikiana wapeleke malalamiko yao Taswa na MCT kwa hatua zaidi za usuluhishi.
Na Elizabeth Edward,Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post