KANGI LUGOLA AMPA MIEZI MINNE LUGUMI

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola ametoa onyo kwa mfanyabiashara Said Lugumi baada ya kumpa miezi minne ya kukamilisha makubaliano ya mkataba kati ya kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi.



Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani, jijini Dar es Salaam jana Jumanne Julai 31, 2018 Waziri Lugola alisema kuwa mahakama ya kushughulikia kesi za rushwa iliyoanzishwa na Rais Dkt.Magufuli bado haijapata wateja wakati ni wengi wanaoiba fedha za serikali.


“Mahakama ya kushughulikia kesi za rushwa inakosa wateja,na wanaoibia serikali wapo wengi mtaani,na kutokana hili Saidi Lugumi nimempa miezi minne kukamilisha makubaliano ya mkataba na akishindwa atakuwa mteja wa mahakama hiyo” amasema Lugola.


Aidha Waziri Lugola aliongeza kuwa mkataba unaomhusu mfanyabiahashara Said Lugumi bado unafanyiwa uchunguzi na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) na baada ya uchunguzi hatua sitahiki zitachukuliwa.


Ikumbukwe kuwa mfanyabishara huyo aliingia katika msuguano na serikali mwaka 2016, ambapo kamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC) ilibaini ubadhilifu katika mkataba kati ya kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi chini ya Mkuu wa jeshi la polisi wakati huo Ernest Mangu.


Mkataba huo ulisainiwa kwa ajili ya kufungwa kwa mashine za utambuzi wa alama za vidole (AFIS) kwenye vituo 108 kwa gharama ya shilingi bilioni 37 ambapo kampuni hiyo ilifunga mashine hizo kwenye vituo 14 tu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527