RC MPYA AJIAPIZA KUWA YUPO TAYARI KUTUMBULIWA NA JPM | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, August 7, 2018

RC MPYA AJIAPIZA KUWA YUPO TAYARI KUTUMBULIWA NA JPM

  Malunde       Tuesday, August 7, 2018
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla huku akijiapiza kuwa yuko tayari kutumbuliwa na Rais kama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, hawatakubali kuondoa makundi na kupoteza tena Jimbo la Mbeya Mjini.

Chalamila alitoa kauli hiyo wakati wa makabidhiano hayo jana na kudai kuwa kwa mtazamo wake anaona jimbo hilo kwa sasa lipo wazi na linaweza kurejea katika himaya ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

CCM ililipoteza kwa mara ya kwanza jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, Polisya Mwaiseje (NCCR-Mageuzi) alipomshinda Bruno Mpangala, lakini ikalirejesha mwaka 2000 kupitia kwa Benson Mpesya.

Mwaka 2010, Mpesya aliangushwa na Joseph Mbilinyi 'Sugu' (Chadema) anayeendelea kuliongoza hadi sasa.

Katika makabidhiano hayo, Chalamila alisema kuwa pamoja na mtazamo wake huo wa uwezekano mkubwa wa kulirejesha CCM jimbo hilo, wanachama wa CCM wasishangae kushindwa tena ikiwa wataendelea na makundi makubwa yaliyo ndani ya chama hicho.

Alisema amekuwa akifuatilia migogoro ya CCM Mbeya tangu alipokuwa Iringa na amebaini kuna makundi makubwa ambayo yanaweza kukigharimu chama hicho.

“Endapo nitaondolewa kwa sababu ya CCM kupoteza jimbo hili, nitarudi kulima, nitamshukuru Rais na nitamwambia kuwa sijasikitika," Chalamila alisema na kuongeza:

"Kama mtataka ushirikiano wa kujenga, mimi kama kamisaa wa chama, nitawapa lakini kama ni ushirikiano wa kuvurugana sitawapa."

Aliongeza kuwa msimamo wake ni kufanya kazi bila kuingiliwa na kiongozi yeyote na yeyote atakayetaka kuingilia majukumu yake atamtaka kusoma katiba na miongozo ya chama.

Chalamila alimshauri Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Jacob Mwakasole na timu yake kuhakikisha wanapambana na kuyaondoa mapema makundi yaliyokivuruga chama hicho.

Alisema kuwa atakuwa tayari kutoa ushauri na kama wataona ushauri wake haufai, atawaacha na hatawaingilia katika uamuzi wao.

Kiongozi huyo wa serikali aliongeza kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Mkoa Mbeya wamefarakanishwa kwa itikadi za kisiasa zilizokuwa zinasababishwa na baadhi ya viongozi.

Alimpongeza Makalla kwa jitihada alizozionyesha kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hasa Mbarali na Rungwe.

Awali, Makalla ambaye amehamishiwa Mkoa wa Katavi, alimweleza Chalamila kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne, alikuwa anapambana na migogoro ya ardhi ambayo ndiyo ilikuwa changamoto kubwa mkoani humo.

Alisema baadhi ya migogoro alishaimaliza ikiwamo ya wananchi waliohamishwa wakati wa upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Wananchi hao walikuwa wanalalamika kupunjwa malipo ya fidia.

“Nakuhakikishia kuwa tumeshirikiana na wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wengine wakiwamo wa dini kumaliza baadhi ya changamoto, lakini nitakukabidhi baadhi ya migogoro ya ardhi kwa maandishi ili uendelee kuitatua,” alisema.

Makalla aliwataka wananchi na viongozi wa Mbeya kumpa ushirikiano Chalamila kama walivyofanya kwake wakati akiuongoza mkoa huo unaosifika kwa uzalishaji wa nafaka.
Chanzo- Nipashe
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post