BWEGE AMTULIZA ZITTO KABWE


Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara maarufu Bwege amemtuliza Zitto Kabwe, akimtaka kutokuwa na wasiwasi licha ya Jeshi la Polisi kufungua jalada la uchunguzi dhidi yake.

Jana Agosti Mosi, 2018 msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa alisema wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya mbunge huyo wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), ikielezwa kuwa alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya viongozi wa Serikali.

Kauli hiyo ya polisi imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kumtaka Zitto kujisalimisha polisi kwa kuwa ametoa kauli za uchochezi wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Kilwa Kusini, mkoani Lindi.

Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Agosti 2, 2018 Bwege amesema Zitto hana makosa kwa kuwa alimualika jimboni kwake kuzungumza na wananchi, si kuandaa mkutano.

“Kama makosa ninayo mimi niliyemualika Zitto. Pale hakuna kesi yoyote ngoja tuone huo uchunguzi wao utasema nini,” amesema Bwege.

Bungara ameeleza namna alivyohojiwa na polisi Julai 30, 2018 siku moja baada ya kufanyika kwa mkutano huo katika viwanja vya Garden ya Mkapa Kilwa Masoko.

Amesema polisi walimhoji mambo mawili, “kwanza ni kwanini alimualika Zitto kuhutubia mkutano wangu wakati si mbunge wa eneo hilo. Waliniuliza njia niliyotumia kumualika, nikawajibu nilimuandikia barua.”

“Niliwaeleza kuwa Zitto alikuja kama mbunge mwenzangu na sio kiongozi wa chama. Walinieleza kuwa sikufuata utaratibu kwa sababu kibali changu cha mkutano sikueleza ujio wa Zitto.”

Baada ya kauli la Lugola, Zitto alijibu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, akibainisha kuwa atakwenda ikiwa atapewa wito wa kisheria.

Ameandika, “waziri hana hayo mamlaka. Kama polisi wananitaka watoe wito wa kisheria nitakwenda.”

“Nitaendelea na kampeni za ubunge wa Buyungu ambapo tunamuunga mgombea wa Chadema na madiwani wa ACT-Wazalendo kwenye kata kadhaa. Nashauri waziri ampate kwanza yule mbwa wa polisi bandari.”

Na Bakari Kiango, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527