AJALI YA GARI YAUA WATU WAWILI,KUJERUHI WAWILI SHINYANGA...RPC AONYA ULEVI,MWENDOKASI


Watu wawili wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wanasafiria lenye namba za usajili T.903 BSF aina ya Toyota Premio kugonga kingo za barabarani kisha kupinduka katika  barabara kuu ya Shinyanga - Mwanza eneo la kijiji na kata ya Bubiki tarafa ya Mondo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Jumapili Agosti 5,2018 majira ya saa nane usiku katika barabara kuu ya Shinyanga kuelekea Mwanza eneo la kijiji na kata ya Bubiki.

Akielezea kuhusu ajali hiyo,Kamanda Haule amesema gari hilo mali ya Mpakani Kassim Kalinga likiendeshwa na Denis Simon Mapunda (36) mkazi wa Morogoro liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya dereva na abiria mwanaume ambaye hajafahamika jina wala makazi yake.

Amesema mbali na vifo hivyo pia watu wawili walijeruhiwa ambao ni Muhsin Hassan (33) aliyeumia ubavuni upande wa kushoto na mwingine ni mwanaume ambaye bado hajafahamika jina wala makazi yake na ameumia sehemu mbalimbali za mwili.

Kamanda Haule ameeleza kuwa majeruhi hao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na hali zao siyo nzuri na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Kamanda Haule amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni ulevi na mwendokasi kulikosababisha dereva kushindwa kulimudu gari na kwenda kugonga kingo za barabara kisha kupinduka na kuongeza kuwa gari husika lipo kituo cha polisi.

“Natoa wito kwa madereva kufuata sheria,taratibu na kanuni za usalama barabarani,kuacha kuendesha vyombo vya usafiri kwa mwendo kasi au wakiwa katika hali ya ulevi”,amesema Kamanda Haule.

“Pia nitoe rai kwa abiria wawapo katika vyombo vya usafiri kutowafumbia macho madereva pale wanapoona vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao safarini,badala yake waendelee kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mapema za makosa ya usalama barabarani na uhalifu mwingine ili wale wote wanaokiuka sheria waweze kushughulikiwa mapema kabla ya madhara kutokea”,ameongeza Kamanda Haule.

Na Kadama Malunde – Malunde1 blog
Gari likiwa eneo la ajali









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527