WAZIRI MKUCHIKA AAGIZA HALMASHAURI KUTENGA MAENEO YA KUANZISHA VITUO VYA URASIMISHAJI NA UENDELEZAJI BIASHARA


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kituo Kimoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ambaye alifungua kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt.George Mkuchika jana
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akisoma hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt.George Mkuchika, katika hafla ufunguzi wa wa Kituo Kimoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, iliyofanyika jana.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Kapteni Mstaafu George Mkuchika ameziagiza halmashauri zote nchini kutenga maeneo ya uanzishwaji vituo vya urasimishaji biashara kwa wananchi ili waweze kuondokana na umaskini.

Agizo hilo limetolewa na kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga katika uzinduzi wa kituo kimoja cha urasimishaji na uendelezaji biashara katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Amesema MKURABITA ndio nyenzo muhimu ya kuwawezesha, kuibua na kuendeleza uwezo wa wananchi kuwa wawekezaji wa ndani wanaowajibika kutengeneza mtaji, soko, ajira na kujenga uchumi wa viwanda ndani ya mfumo rasmi, hivyo ipo haja kwa halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya vituo vya urasimishaji biashara ili kuwasaidia wananchi.

“ Ni matumaini yangu kuwa vituo vya kurasimisha biashara vitatumika pia kutambua na kuzitumia fursa za uwekezaji ambazo zinatengenezwa na kuimarishwa, nitumie fursa hii kuzitaka Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishwaji wa vituo hivi katika kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda vinavyomilikiwa na wananchi” alisema Kiswaga akisoma hotuba ya Waziri Mkuchika .

Aidha, amewahamasisha wafanyabiashara na wananchi wote mkoani Simiyu kutumia huduma zipatikanazo katika vituo vya kusajili na kuendeleza biashara zao, huku akiwasisitiza wafanyabiashara wadogo kama mamalishe, wamachinga na waendesha bodaboda kutumia Kituo cha Bariadi, ili waweze kujiondoa katika mfumo usio rasmi na kuingia katika mfumo rasmi wa uchumi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA Daniel Ole Njoolay ameiomba Serikali kutoa nyenzo za kutosha za kusukuma urasimishaji na uendelezaji wa biashara kukuza mitaji ya wafanyabiashara kwa kuwa hadi sasa utafiti unaonesha kuwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya biashara si rasmi.

Mwenyekiti Mstaafu wa mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) John Chiligati ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu hususani Bariadi kutumia hati miliki za kimila kama dhamana ya kupata mikopo ya kuendeleza kilimo, kuanzisha viwanda na biashara.

Mtendaji mkuu wa MKURABITA Seraphia Mgembe amewashukuru wote waliopata mafunzo ya urasimishaji na uendelezaji wa biashara na kuahidi kuwafuatilia na kuhakikisha kuwa miaka ijayo waweze kufanikiwa kiuchumi.

Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya urasimishaji na uendelezaji wa biashara wameishukuru Serikali kwa mpango huo kuanzisha mradi wa kituo kimoja cha urasimishaji na uendelezaji biashara, kupitia MKURABITA na kuomba waendelee kupewa mafunzo ili wawze kunufaika na biashara zao.

“Tunaomba tuendelee kupigwa msasa zaidi na zaidi ili tuweze kutunza mahesabu ya biashara zetu vizuri, tuweze kulipa kodi na kuendeleza biashara zetu katika mfumo ulio rasmi” alisema Mashaka Than mfanyabiashara kutoka Bariadi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bw. Melkizedeck Humbe Kituo Kimoja cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichofunguliwa Julai 26, 2018 kitatoa huduma za leseni za biashara, usajili wa biashara, huduma za kibenki, TRA, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wakala wa vipimo na huduma za kampuni binafsi ya GODTEC.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527