WAZIRI LUGOLA AMBANA MBAVU IGP


Kushoto ni Waziri Lugola, Kulia ni IGP Simon Sirro

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mh. Kangi Lugola, ametoa muda wa siku 14 kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Simon Sirro kufika ofisini kwake kumueleza mikakati ya kuwawezesha Watanzania kufanya kazi kwa saa 24 ikiwa ni pamoja na kuzuia matishio ya mabasi kutembea nyakati za usiku.

Waziri Lugola ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika makao makuu ya kikosi cha kutuliza ghasia kilichopo Ukonga Jijini Dar es Salaam na kuongea na Askari wa Kikosi hicho na wale wanaohudumia katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere.

Wakati akitoa agizo hilo, Mhe. Lugola amesema kuwa ili kufikia Uchumi wa kati Watanzania wanatakiwa kufanya kazi za kiuchumi kwa masaa 24 hivyo IGP anapaswa kumhakikishia mikakati ya jeshi lake katika ushiriki wao wa kuwapatia watanzania usalama kwa muda wotewakifanya shughuli hizo za kiuchumi.

"Nataka IGP aje aniambie kwamba je, jeshi la polisi limesalimu amri kwa majambazi ndiyo maana mabasi hayatembei usiku, lakini biashara mbalimbali ikifika saa 12 zinafungwa, ukiuliza unaambiwa ni kwa sababu ya usalama, nataka IGP aniambie kama majambazi ndio wanaotupatia amri...Hatuwezi kukubali kupewa amri na majambazi ni masaa mangapi tunatakiwa kufanya shughuli za kiuchumi au kupangiwa maeneo ya kwenda na wapi tusiende," Waziri Lugola.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527