Wednesday, July 11, 2018

WAZIRI KALEMANI AZINDUA MRADI WA UMEME VIJIJINI - REA III KATIKA VIJIJI 149 KIGOMA

  Malunde       Wednesday, July 11, 2018
Waziri wa Nishati Medadi Kalemani amewaagiza wasimamizi wa mradi wa umeme Vijijini REA pamoja na TANESCO kuanzisha madawati ya kutoa huduma na vituo vidogo vya shirika la Umeme Tanzania kwa kila kata  nchi nzima kwa ajili ya kutatua kero za wananchi na kuhakikisha ifikapo Juni 2021 kila kijiji na kila mwananchi anapata umeme.


Maagizo hayo aliyatoa jana katika kijiji cha Rusesa wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma, wakati wa uzinduzi wa REA  awamu ya Tatu katika vijiji 149 vya wilaya nne za mkoa wa Kigoma ambazo zilichelewa kupata  mradi huo, ambapo aliwataka wasimamizi wa TANESCO na mawakala wa Umeme vijijini REA kumsimamia Mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo mchana na usiku kuhakikisha wananchi wanapata umeme kwa wakati kutokana na wananchi hao kuwa na hamu ya kupata umeme.


Alisema  TANESCO inatakiwa kuanzisha ofisi ndogo katika kila kata na dawati la kusikiliza kero za wananchi ili kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya serikali ya shilingi 27,000/= bila kuibiwa na wananchi wapate eneo la kupeleka kero zao ili kuepusha kero na kuhakikisha umeme katika kata unawekwa kwenye vijiji vyote na vitongoji vyote vilivyokusudiwa kama serikali ya awamu ya tano ilivyokusudia kwa kila kijiji kupata umeme.

"Fananisheni umeme huu na treni ambayo mmezoea kuipanda na kila mwananchi ataipanda treni hii ya umeme, mmechelewa kuipanda lakini mtakuwa wa kwanza kufika nimekuja  kufanya kazi kumtambhlisha kwenu mkandarasi na kutoa majukumu yake ya kazi, tulikuwa hatujaanza kutekeleza mradi huu tulianza kwa sehemu ndogo sana katika wilaya ya Kibondo na Kakonko leo tumekuja kupiga hodi katika wilaya nne zilizokuwa zimebaki", alisema Waziri  huyo.

" Niwaombe wananchi muitunze miundombinu hii itakayowekwa, serikali imetumia gharama kubwa sana kuwekeza katika miundombinu hii, na nitoe wito kwa wakandarasi kuwatumia vijana wa mkoa wa Kigoma katika utekelezaji wa mradi huu  kwa kuwa Rais ametoa bilioni 54 kwa ajili ya mradi huu kutekeleza ahadi yake aliyoahidi wakati wa uchaguzi ,lazima wananchi wanufaike na mradi huu na vijana wapate ajira ", alieleza Waziri Kalemani.

Aidha aliahidi kuuunganisha mkoa wa Kigoma na gridi ya Taifa kufuatia maombi yaliyotolewa na wabunge wa mkoa huo na kuwataka wasimamizi wa mradi huo kuweka umeme katika maeneo yote ya taasisi za umma pamoja na maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda na uwekezaji ili kuinua uchumi wa wananchi wa mkoa wa Kigoma.


Akizungumzia mradi huo ,Mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini REA,Amos Maganga alisema mradi uliozinduliwa ni mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa kwanza, ni muendelezo wa  miradi iliyo tangulia ambapo Kigoma  mradi wa Rea awamu ya tatu  ulianza kwa wilaya za Kakonko na Kibondo miezi miwili iliyopita.


Alisema mzunguko wa kwanza  wa Awamu hii ya tatu utaanza na vijiji 80 vya wilaya ya Buhigwe, Kasulu ,Uvinza na Kigoma Vijijini na mradi huo utapita katika  vijiji 149  na vijiji hivyo vinakamilisha idadi ya vijiji 195 vyenye  umeme kati ya vijiji 306 vya mkoa mzima  na  111 vimeanza kusanifiwa ili na vyenyewe vianze kupata Umeme kuanza Julai 2019 .

Awali akimkaribisha waziri kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kigoma ,Mkuu wa wilaya ya Buhigwe na Kasulu , Brigedia Jenerali Marco Gaguti  alisema kila walipokuwa wakipita katika maeneo ya utendaji wananchi walikuwa wakiuliza umeme utafika lini, hivyo anaamini uzinduzi huo sasa ni chachu kwa wananchi kuanzisha viwanda na kuanzisha miradi mbalimbali.

"Katika mpango wa Kigoma ni kwenda kwa spidi ya kukimbia kuhakikisha maendeleo yanakuja kwa kasi kubwa mkoani Kigoma, tumejipanga na tunaamini kwa umeme huu tulioupata Kigoma yetu haitakuwa nyuma tena na kuanza rasmi uwekezaji na uanzishwaji wa viwanda kuunga mkono kauli mbiu ya Rais wa awamu ya tano ya serikali ya Viwanda ", alisema Brigedia Jenerali Gaguti.

Nae Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vuma Holle alisema Wana Kasulu wanamshukuru  sana Rais kwa kukamilisha  baadhi ya ahadi zake alizoahidi wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na umeme, huduma za afya na  barabara, kilichobaki ni huduma za maji kitu kimoja ambacho wananchi wanakisubir kwa hamu ni maji.

Alisema umeme huo ulichelewa kutokana na mkandarasi aliyeomba wa kwanza aligushi nyaraka na kulikuwa na kesi inaendelea mahakamani ambapo Waziri husika amejitahidi kutafuta wanasheria wa serikali wazuri  waliosaidia suala hilo kuisha kwa wakati  na kuomba mradi utakapoanza Wakandarasi kufanya haraka kutekeleza mradi huo na wananchi wa Kigoma wanufaike na mradi huo.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post