UBELGIJI YAITWANGA BRAZIL 2-1.....KOMBE LA DUNIA KUBAKI ULAYA


Wachezaji wa Ubelgiji wakishangilia moja ya mabao yao dhidi ya Brazil


Baada ya Brazil kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ubelgiji kwenye mechi ya robo fainali iliyomalizika usiku huu, sasa imekuwa rasmi bingwa wa mashindano atatokea Bara la Ulaya.

Brazil na Uruguay ambazo zote zinatokea Amerika ya Kusini ndio timu pekee zilizokuwa zimebaki kwenye mashindano ambazo hazitokei bara la Ulaya lakini zote zimeondolewa ikianza Uruguay kwa kuchapwa bao 2-0 na Ufaransa na sasa imefuata Brazil.

Katika mchezo uliomalizika, Ubelgiji imeweka rekodi ya kucheza mechi 25 bila kufungwa huku pia ikiwa ndio timu yenye wachezaji wengi waliofunga mabao kwenye fainali hizi wakifika 9 ikizidiwa na Ufaransa mwaka 1982 na Italia mwaka 2006 ambapo walifunga wachezaji 10 tofauti.

Kwa upande wa Brazil, wao wameendelea na rekodi mbaya dhidi ya timu za Ulaya ambapo imeondolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia za hivi karibuni mara 4 na timu kutoka bara la Ulaya.

Wachezaji wa Ufaransa wakishangalia bao dhidi ya Uruguay leo.

Iliondolewa na Ufaransa mwaka 2006, Uholanzi mwaka 2010, Ujerumani mwaka 2014 na Ubelgiji mwaka 2018. Ubelgiji sasa itacheza na Ufaransa kwenye nusu fainali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527