TUNDU LISSU KUFANYIWA UPASUAJI MWINGINE

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kesho Julai 7, 2018 atafanyiwa upasuaji wa mwisho utakaomwezesha kutembea bila msaada wa magongo.


Ujumbe wa Lissu alioutoa leo Julai 6, 2018 kutoka nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu, ameeleza safari ya matibabu yake inavyoendelea hadi sasa.


Lissu, aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu anafanyiwa upasuaji huo ikiwa ni mwendelezo wa matibabu anayopatiwa tangu aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017 akiwa katika makazi yake mjini Dodoma.


“Operesheni ya mwezi uliopita imepona, angalau kwenye muscles (misuli). Mfupa bado una kazi kubwa kidogo na utachukua muda kupona,” amesema Lissu.


“Licha ya maendeleo haya mazuri, bado kuna operesheni moja zaidi inahitajika. Madaktari wangu walipaswa kuniwekea ‘metal frame’ ya kusapoti mfupa uliofanyiwa operesheni mwezi uliopita.”


Mwasheria huyu mkuu wa Chadema amesema, “hata hivyo, hiyo ilishindikana kwa sababu operesheni yenyewe ilichukua saa saba na nilipoteza damu nyingi sana.”


Amesema mguu huo wa kulia uliumizwa sana kwa risasi, “ulivunjwa sehemu mbili na mfupa wa juu ya goti uliharibiwa. Kazi ya kuurekebisha ni ngumu sana kwa sababu hiyo.”


“Madaktari wa Nairobi (Kenya) na wa hapa (Ubelgiji) wamefanya kazi kubwa kuhakikisha wanautibu vizuri mpaka sasa naweza kusimama na kutembea, hata kama ni kwa kuchechemea kwa magongo.”


Amesema upasuaji huo atafanyiwa kesho asubuhi ili kukamilisha tiba ya mguu huo na kwamba akipona ataweza kutembea bila msaada wa mgongo.


“Madaktari wangu wameniambia kwamba hiyo ‘metal frame’ itakaa mguuni kati ya miezi sita hadi nane. Hata hivyo, haina maana kwamba nitakaa hospitalini kwa muda wote huo,” amesema.


“Haina maana kwamba sitaweza kufanya kazi yoyote ile katika kipindi hicho. Kwa kushauriana nao, pamoja na nyie ndugu, familia na jamaa zangu na viongozi wenzangu, tutaangalia mambo ninayoweza kuyafanya wakati nikiwa kwenye safari ya full recovery.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527