SIMBA HATARINI KUTOKAMILISHA USAJILI


Kushoto ni kocha mpya wa Simba (Patrick Aussems) na kulia ni kaimu Rais wa Simba Salim Abdallah.

Klabu ya soka ya Simba huenda ikashindwa kukamilisha usajili wa kiungo mkongwe wa Mtibwa Sugar Hassan Dilunga, kutokana na kutofikia makubaliano na klabu yake mpaka sasa licha ya awali kuelezwa kuwa nyota huyo amesaini Simba kwa miaka miwili.

Akiongea na www.eatv.tv Dilunga amesema meneja wake ameshaongea na Simba wakakubaliana kila kitu ila suala hilo sasa limebaki kwa upande wa klabu yake ya Mtibwa Sugar na Simba ambao bado hawajamalizana.

''Simba wameshanifuata tukaongea kuhusu mahitaji yangu binafsi tukakubaliana lakini bado nina mkataba na Mtibwa Sugar siwezi kujiunga nao hivihivi mpaka wamalizane na timu yangu ndio inipe ruhusa ya kuondoka'', - amesema.

Kwa upande mwingine kocha wa Mtibwa Sugar Zuberi Katwila amesema yeye bado anamtambua Dilunga ni mchezaji wa Mtibwa ndio maana yupo kwenye programu zake za mazoezi yanayoendelea kwenye uwanja wa Lugalo jijini Dar es salaam.

Mchezaji Hassan Dilunga alipokuwa akisaini mkataba na Mtibwa Julai 2017.

Kwa upande wa Simba kupitia kwa msemaji wake Haji Manara wamegoma kueleza kama wamefikia makubaliano na Mtibwa huku akieleza kuwa wanaendelea na zoezi la usajili na pindi watakapokamilisha watatoa orodha ya wachezaji waliowasajili.

Julai 18 mwaka huu, Mtibwa Sugar ilikamilisha usajili wa mchezaji Juma Luizio kutoka Simba. Luizio amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Mtibwa Sugar ambayo ndio timu iliyolea kipaji chake tangu akiwa kinda.
Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527