SHEIKH ABARIKI SHERIA YA KUOLEWA UKIWA NA UMRI WA MIAKA 15



Katibu wa Baraza la Maulamaa liliopo chini ya BAKWATA nchini Tanzania, Sheikh Hassan Saidi amedai hawaoni haja ya kubadilishwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hasa katika kipengele cha umri kwa kuwa watoto hao wanafundishwa somo la ndoa tokea wakiwa shuleni, licha ya sheria hiyo kupingwa na jamii pamoja na wanaharakati mbalimbali kusudi ibadilishwe.

Katibu huyo ametoa mtazamo wake huo wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa BreakFast inayorushwa na East Africa Radio leo Julai 27, 2018 baada ya Mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni nchini Tanzania (TECMN), kutoa takwimu zake kuwa watoto wa kike 36 kati ya 100 wanaolewa na kuzaa chini ya umri wa miaka 18 kila mwaka.

"Sisi hatuoni kwamba sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hivyo ilivyo kwamba inahitaji kubadilishwa kwasababu kuna mazingira yaliyokuwa muhimu yanatakiwa yasaidiwe ili sheria hiyo iweze kutekelezwa. Hatuoni haja ya umri ya kubadilishwa, hii habari ya tendo la ndoa inaanza mapema sana ndio maana hata katika kupambana na UKIMWI, tunaona kwamba ni bora kuwapa kondomu wakiwa shuleni inamaana kwamba tunakubaliana na ndoa za utotoni wakiwa shuleni ndio maana wanapewa elimu ya ngono na kondomu", amesema Sheikh Hassan.

Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 imekuwa gumzo kwa kipindi kirefu huku wanaharakati mbalimbali wakipigia kelele iweze kubadilishwa ili kusudi watoto wa kike waweze kupata haki zao za muhimu kama kusoma na vitu vingine kama wapatavyo watoto wa kiume.

Sheria hiyo ya ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu msichana mwenye umri wa miaka 15 kuolewa na mwanaume endapo atapatiwa ruhusa kutoka kwa wazazi wake jambo ambalo kwa sasa limekuwa likipingwa, kwa kuwa watoto hao mifumo yao ya uzazi inakuwa haijakomaa pamoja na suala la kiakili katika kumudu majukumu ya ndoa, jambo ambalo wanaharakati wameiomba serikali ibadilishwe sheria hiyo iwe juu ya miaka 18.

Julai 26, 2018 Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuainisha maeneo yote ambayo sheria zake zina matatizo na itolee mapendekezo yatakayosaidia serikali kurekebisha sheria mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa wananchi na maendeleo ya Taifa.
Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527