SERIKALI YA TANZANIA YATISHIA KUIADHIBU TWAWEZA KUFANYA UTAFITI 'BILA KIBALI'

Wachangiaji na wadau mbalimbali wameshiriki kuchambua Utafiti uliotolewa na Twaweza

Serikali ya Tanzania imeitaka taasisi ya utafiti isiyo ya kiserikali ya Twaweza kueleza ni kwa nini ilifanya utafiti kuhusu maoni ya wananchi 'bila kibali'.

Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeiandikia taasisi barua na kuitaka ieleze ni kwa nini haifai kuchukuliwa hatua za kisheria.

Barua hiyo inasema Twaweza waliwasilisha maombi ya vibali vya kufanya utafiti awali nchini Tanzania lakini utafiti huo wa Sauti ya Wananchi haukujumuishwa.

"Mwishoni mwa wiki kulikuwa na taarifa kuhusu utafiti mpya wa Twaweza kwa jina Sauti za Wananchi.

Kwa kuwa tume hii haina rekodi zozote kwamba ilitoa kibali kwa Twaweza au kuna ombi la kibali cha utafiti kama huo ambacho kiliwasilishwa, kuchapishwa kwa matokeo ya utafiti huo kunakiuka kifungu 11 cha Mwongozo wa Kusajiliwa na Kuidhinishwa kwa Usajili wa Kitaifa kwa kutoandikisha mradi huu wa utafiti kwa Costech."

Twaweza wamethibitisha kwamba wameipokea barua hiyo lakini bado hawajatoa tamko rasmi.

Utafiti huo wa Twaweza ulikuwa unasema asilimia 65 ya wananchi Watanzania walisema hawako tayari kutumia njia ya maandamano kuishinikiza serikali katika mambo yasiyowaridhisha.

Kwa upande mwingine, mwananchi mmoja kati ya wanne (27%) ana uwezekano wa kushiriki kwenye maandamano.

Ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2016, idadi ya wanaosema wana uwezekano wa kushiriki ilishuka kidogo sana (kutoka 29% mpaka 27%) wakati ambao wanasema hawana uwezekano wa kushiriki imeongezeka (kutoka 50% mpaka 65%).

Wananchi wachache kwa hiari walitaja maandamano kama njia ya kufikisha malalamiko yao kwa serikali. Idadi kubwa ya wananchi walisema hawako tayari kushiriki kwenye maandamano kuhusu jambo lolote lisilowapendeza.- ikiwemo idadi kubwa ya wafuasi wa vyama vya upinzani.

Na wananchi wengi zaidi wanaunga mkono serikali kukataza mikutano na maandamano ya kisiasa kuliko wale wanaopinga.

Utafiti wa Twaweza ulitaja sababu kadhaa za kutofanyika maandamano ya tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 2018 kama yalivyokuwa yamepangwa na mwanaharakati Mange Kimambi.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa umaarufu wa Rais John Magufuli umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 55 mwaka huu.Haki miliki ya pichaIKULU TANZANIAImage captionRaisi wa Tanzania Dkt John Magufuli

Asilimia 55 ya wananchi wanaukubali utendaji wa Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani mwaka 2015. Kukubalika huku kumepungua kutoka 96% mwaka 2016, na 71% mwaka 2017.

Kiwango cha kukubalika kwa Rais kimeshuka kutoka kwenye rekodi ya juu kuwahi kuwekwa na Rais wa Tanzania mpaka rekodi ya chini tangu takwimu hizi zianze kukusanywa mwaka 2001.

Msemaji na katibu mwenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Bwana Humphery PolePole alikosoa utafiti huo wa Rais Magufuli bado ni maarufu sana nchini Tanzania kutoka na sera zake.
Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527