RAIS MAGUFULI AWATUNUKU KAMISHENI MAAFISA WA JWTZ

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 123 wa Jeshi la Ulinzi na Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika cheo cha Luteni UsO.

Rais Magufuli amewatunuku Kamisheni Maafisa hao wapya wa Jeshi la Ulinzi na Wananchi wa Tanzania kwa cheo cha Luteni Usu ambao walikuwa wanafunzi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi, kilichopo Monduli Arusha leo [Jumamosi Julai 7, 2018] katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo hicho, Luteni Generali Paul Massao Maafisa waliohitimu kozi ya 63 mwaka 2017 jumla yao ni 123 kati yao 118 ni watanzania, na wahitimu 5 kutoka nchi za Uganda, eSwatini, na Rwanda.


“Kati ya Maafisa watanzania 118 wanawake ni 3 na wanaume 115, ambapo Maafisa 121 walipata mafunzo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Mondulu na Maafisa wa 2 walipata mafunzo yao nchini India” alifafanua Luteni Generali Massao.


Sambamba na kuwatunuku Kamisheni Maafisa hao kwa cheo cha Luteni Usu, Rais Magufuli ametoa zawadi kwa wahitimu waliofanya vizuri ambao ni Emmanuel Kakuba Afisa aliyefanya vizuri zaidi darasani, Danie Meshack aliyefanya vizuri zaidi kwenye mafunzo, na katika medani ni Ramadhan Kakombe.


Wengine, ni Amstrong Mwamwesige kutoka Uganda aliyefanya vizuri kutoka nchi rafiki pamoja na Beatrice Kipinge ambaye ni mwanamke aliyefanya vizuri zaidi.


Aidha, wahitimu 87 waliachishwa mafunzo kwa sababu mbalimbali ikiwemo magonjwa, utovu wa nidhamu ama mtu kuomba kwa hiari yake.


Hafla hiyo ya kutunuku Kamisheni kwa Maafisa wa ilipambwa na burudani kutoka vikundi mbalimbali ikiwemo kikundi cha ngoma za asili pamoja na kikundi cha mziki wa dansi cha Jeshi cha Mondulu jijini Arusha.


Aidha, tangu kuingia kwake madarakani mwaka 2015 hii ni mara ya 6 ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwatunuku Kamisheni Maafisa wa Jeshi la Ulinzi na Wananchi Tanzania (JWTZ).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527