TAJIRI WA MABASI AWATWANGA RISASI YA TUMBO,MIGUU MAOFISA USALAMA WA TAIFA


Mfanyabiashara maarufu nchini, Peter Zacharia (pichani) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara kwa tuhuma za kuwapiga risasi maofisa wawili wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), wakati wakiwa katika shughuli zao za kikazi.


Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ni mmiliki wa mabasi ya Zacharia yanayofanya safari za Musoma, Tarime na maeneo mbalimbali ya nchi.

Zacharia anadaiwa kuwajeruhi maofisa hao ambao mmoja amepigwa risasi ya tumboni na mwingine kujeruhiwa kwenye miguu na mikononi walipofika eneo lake la biashara.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, alisema maofisa hao wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi walipigwa risasi juzi majira ya saa tatu usiku.

Akisimulia tukio hilo, Malima alisema gari lao lilisimama katika kituo chake cha kuweka mafuta likiwa na watu wawili na waliposhuka, Zacharia alitoka ofisini kwake na ndipo milio ya risasi ilianza kusikika.

“Gari ilisimama kwa ajili ya kuweka mafuta katika kituo chake cha mafuta baadaye ikaonekana wale maofisa wawili wa usalama wa taifa ambao walishuka kwenye gari wamepigwa risasi na Zacharia,” alisema na kuongeza:

“Kwenye gari kulikuwa na maofisa wengine ambao walikuwa wote kwenye ratiba za kikazi walishuka chini na kumdhibiti Zacharia na kumpeleka polisi,” alisema Malima.

Alisema maosifa wawili wa usalama wa taifa walijeruhiliwa vibaya na wanaendelea na matibabu mkoani Mara.

“Nimetoa kauli hii kwa sababu kila mtu ameanza kusema la kwake kulikuwa na jaribio la kufanya fujo haya ni mambo ambayo ni lazima tuwekane sawa,” alisema Malima.

“Kwanza kabisa hii nchi inatawaliwa na mfumo wa sheria na sheria ipo pale pale sasa hivi Peter Zacharia yupo kwenye mikono ya sheria chini ya polisi Kanda Maalum ya Tarime na wale wengine wako kwenye utaratibu wa kupatiwa matibabu,” alisema.

Nipashe ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime /Rorya, Henry Mwaibambe, ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea.

Chanzo kimoja mkoani humo kimeliambia Nipashe kuwa maofisa hao waliojeruhiwa wamesafirishwa kwa ndege ya jeshi kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

“Hali zao si nzuri na wamepelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, mmoja ambaye amepigwa risasi ya tumbo ndiye anaonekana kuwa katika hali mbaya zaidi,” kilisema chanzo hicho.

CHANZO - NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527