NDOA YA KAKA NA DADA YASAMBARATISHWA | MALUNDE 1 BLOG

Monday, July 16, 2018

NDOA YA KAKA NA DADA YASAMBARATISHWA

  Malunde       Monday, July 16, 2018

Wasaidizi wa kisheria wamefanikiwa kuisambaratisha ‘ndoa feki’ inayodaiwa kuwa ya mtu na kaka yake wa kuzaliwa katika Mtaa wa Matindigani, Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi, baada ya mke halali wa ndoa kufukuzwa yeye na wanawe wawili. 

Mama huyo wa watoto wake wawili alifukuzwa na mumewe (jina limehifadhiwa), baada ya kujifungua mtoto wa pili.

Akitoa ushuhuda wake kuhusu kazi iliyofanywa na wasaidizi hao kutoka Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Moshi Mjini (Washemom), Elisiana Mwanja, alidai mumewe alichukua uamuzi huo, baada ya kumuita dada yake aje kumhudumia kwa wiki moja.

“Baada ya kumaliza uzazi katika kipindi kilichozidi miezi mitatu, mume wangu aliniambia niende nyumbani kwa wazazi wangu Singida, nikamkatalia, lakini akanisisitiza kwamba nirudi nyumbani kwetu kuna shughuli ataenda kufanya huko na nikimaliza ningerejea kwake.

“Nilipokubaliana nae, akaniambia nimwandikishe chekechea huko huko Singida mtoto wetu wa kwanza, nilikaa huko kwa miezi sita; ndio nikapata taarifa kwamba wifi yangu yuko kwenye mji wangu na anaishi na mume wangu. Baada ya mwaka mmoja, ndugu hao wawili wakiwa kama mume na mke, waliamua kuhama na kwenda kupangisha eneo jingine, baada ya mimi kugundua.”

Aliporejea na kuhoji hali hiyo, mumewe aliamua kuuza mazao yote ya chakula waliyokuwa wamevuna shamba walilolima pamoja na kumfukuza akimwambia arudi kwao Singida.

“Niliteseka na wanangu na alipouza vyote, akaniambia rudi Singida hapa hamna chako na yeye na huyo dada yake wakachukua vitu tulivyonunua pamoja. Kutokana na hiyo hali, nikalazimika kuondoka na kwenda kukaa kwa ndugu yangu kwa miezi miwili, na nikiwa huko nikashauriwa niwaone wasaidizi wa kisheria watanisaidia,"alisema.

Kwa mujibu wa Mwanja, alipochukua jitihada za kwenda kuwaona wasaidizi hao wa kisheria, walimwita mumewe wakaongea naye, akajitambua amefanya makosa na akaomba mkewe aende Singida akamchukue mtoto nyumbani kwao alikokuwa ameachwa na akasaidiwa kumtafutia mwanawe shule na hivi sasa ameaanza darasa la kwanza mwaka huu.

Akielezea furaha yake, Mwanja aliwashukuru wasaidizi hao wa kisheria kwa kufanikisha kumbana mumewe na kukubali kutoa matumizi ya watoto, kumfungulia mkewe biashara, kuhudumia familia yake na kurudi kwenye ndoa yao akiwa ameachana na dada yake.

Ofisa Mwandamizi wa Kitengo cha Ufuatiliaji, Tathmini na Taarifa wa Shirika la Kilimanjaro Women Information Exchange and Community Organization (Kwieco) ambalo ni walezi wa wasaidizi hao wa kisheria, Peter Mashingia, alisema jamii ambayo watu wake wanafahamu masuala ya sheria na haki za binadamu inayo nafasi kubwa ya kupiga hatua ya maendeleo kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Alisisitiza kuwa utii wa sheria na ulinzi wa haki za binadamu, huwawezesha wanawake kufurahia fursa sawa na wanaume, huku haki za watoto na jamii za wachache zikilindwa na utu wao kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Chanzo-Nipashe
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post