MWANAMKE MJAMZITO AUAWA KWA KULIWA NA MAMBA AKIOGELEA ZIWA TANGANYIKA

Mkazi wa Kijiji cha Msamba, Kata ya Ninde, wilayani hapa Magreth Ndasi (18), ameuawa kwa kuliwa na mamba wakati akiogelea katika Ziwa Tanganyika.

Akizungumzia tukio hilo, kaka wa marehemu Joseph Ndasi, alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita (Julai 27) majira ya saa 12:30 jioni baada ya Magreth aliyekuwa pia ni mjamzito kwenda kuoga katika ziwa hilo.


Alisema alipofika katika ziwa hilo aliingia ndani ya maji na kuanza kuoga ndipo alipovamiwa na mamba huyo ambaye alimkamata mguu na kuondoka naye kuelekea katika kina kirefu cha maji.


“Wakati alipokuwa anavutwa na mamba huyo alipiga mayowe ya kuomba msaada ndipo walipojitokeza wananchi kutaka kumsaidia,” alisema.


Alisema baada ya mamba huyo kuona kundi la watu likiwa linaingia ndani ya maji, alimzamisha Magreth na kumkalia juu huku akifoka kuwatisha watu waliokwenda kumuokoa.


Aidha, wananchi walioshuhudia tukio hilo, walisema watu wenye silaha za jadi walipofika karibu na mamba huyo ili kumshambulia, alimwachia mwanamke huyo ambaye tayari alikuwa ameshakufa na kukimbia.


Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuacha kwenda kuogelea ziwani hasa nyakati za jioni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527