POLISI WALIOHUSISHWA MAUAJI YA MWANAFUNZI 'AKWILINA' WAACHIWA HURU


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema askari waliokamatwa wakihusishwa na kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini wameachiwa huru.



Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala eneo la Mkwajuni jijini Dar es salaam, wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.


Aprili 20, 2018 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alisema jalada la kesi ya Akwilina amelifunga rasmi, kubainisha kuwa Jeshi la Polisi linapotumia nguvu kuzuia maandamano au vurugu na kusababisha mauaji, haliwezi kushtakiwa.


Leo Jumanne Julai 24, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuulizwa hatima ya askari hao, Mambosasa amesema wameachiwa, “ni kweli kuna askari tulikuwa tunawashikilia kwa ajili ya uchunguzi, upelelezi ulipomalizika imebainika hawahusiki.”

“Wale askari waliachiwa kwa maelekezo ya mwanasheria na ushahidi ulikuwa hafifu wa kuwatia hatiani.”

Awali, Mambosasa amewaonya watumiaji wa barabara kuwa makini na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa madereva wazembe hususan wa bodaboda ambao hawatii alama za barabarani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527