MTOTO WA MIAKA 6 AUAWA KWA KUKATWA PANGA SABABU YA MUWA


Polisi mkoani Iringa inamshikilia Jofrey Josephat (29), mkazi wa Ipogolo wilayani Iringa akituhumiwa kwa mauaji ya mtoto wa miaka sita.

Taarifa ya polisi inasema chanzo cha tukio hilo ni mtuhumiwa kutolewa lugha ya maudhi na mtoto kwa sababu alimnyima muwa.

Inadaiwa mtoto huyo alitamka kuwa mtuhumiwa ni mpumbavu na hafai baada ya kumnyima muwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amesema leo Julai 5, 2018 kuwa Josephat ambaye ni mtunza bustani anatuhumiwa kwa mauaji yaliyotokea jana Julai 4, 2018 saa kumi na moja jioni, eneo la Kibwabwa B, kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa.

Amesema mtoto huyo Prosper Myovela aliuawa kwa kukatwa kwa panga shingoni na mikononi.

Kamanda Bwire amesema mtuhumiwa alitumia panga na baadaye kisu kumkata mtoto huyo na aliuhifadhi mwili kwenye kiroba na kuuficha kwenye nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika.

Amesema upelelezi unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Na Berdina Majinge, Mwananchi
Theme images by rion819. Powered by Blogger.