Picha : SHIRIKA LA ICS LAKABIDHI MRADI WA KISASA WA MAJI WA MALIPO KABLA KATIKA MJI WA MAGANZO SHINYANGA

Shirika la Investing in Childrean and Societies (ICS) limeikabidhi serikali ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla (sustainable prepaid water meter system project) unaotekelezwa katika mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu.

Hafla fupi ya ICS kukabidhi shughuli zote za mradi huo endelevu wa maji kwa serikali imefanyika  Ijumaa Julai 6,2018 katika uwanja wa Maganzo ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi ,Mwakilishi wa Meneja Mkazi wa shirika la ICS Tanzania, Peter Matyoko alisema mradi huo umeanzishwa na shirika la ICS mwishoni mwa mwaka 2015 kwa ufadhili wa shirika la UK Aid kupitia Human Development Innovation Fund (HDIF) kwa lengo la kutoa huduma ya maji kwa wakazi 17,072 wa Mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala ifikapo mwaka 2025.

“Huu ni mradi wa mfano katika matumizi ya malipo kabla (Pre-paid) umegharimu kiasi cha Shilingi billion 1.1 zilizotolewa na wadau watatu ambao ni ICS, Susteq na HDIF na chanzo cha maji ya mradi huu ni maji ya Ziwa Victoria kupitia bomba kubwa la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA)”,alieleza.

Matyoko alisema lengo la mradi ni kuwapunguzia wananchi adha ya kufuata maji umbali wa kutoka kilomita 5 hadi kufikia umbali wa usiozidi mita 400 kama ilivyo katika sera ya Maji ya Taifa ya Mwaka 2002 kwa wakazi.

“Tumekamilisha ujenzi kwa asilimia 100,tumemaliza ujenzi wa bomba la maji lenye kipenyo cha 6’’ na urefu wa 1.3 km kutoka katika bomba kuu la KASHWASA,ujenzi wa mfumo wa bomba za usambazaji maji kutoka kwenye tanki hadi kwenye vituo vya kuchotea maji (water kiosks) 11.7 km,ujenzi wa matanki mawili yenye ujazo wa lita 135,000 na 80,000”alieleza.

“Pia tumejenga vituo 25 vya kuchotea maji vyenye mfumo wa nishati ya jua ( solar power),ufungaji wa dira 25 za mfumo wa ulipaji wa kabla (prepaid water meters) katika kila kituo na ufungaji wa mfumo wa nishati ya jua kwa kila kituo cha kuchotea maji na vituo 11 vya mawakala wa kuuza vocha za maji pamoja na kuwapatia wananchi vifaa vya kuwawezesha kununua Maji kwa njia ya mtandao (tags)”,aliongeza Matyoko.

Aidha aliiomba Halmashauri ya wilaya ya Kishapu kuendeleza Teknolojia hiyo ya maji iliyowekezwa katika mradi huu kwa mujibu wa makubaliano na kwamba ICS itaendelea kushirikiana na halmashauri kwa mambo yanayohusu ushauri ili kutatua changamoto zitakazoibuka muda wowote.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Mfuko wa HDIF, Joseph Manirakiza aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kutoa miongozo mbalimbali juu ya utekelezaji wa mradi huo huku akiwasisitiza wananchi na serikali kutunza mradi huo.

Akipokea mradi huo, Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba alisema mradi huo wa kisasa utasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kutumia maji safi na salama,kupunguza muda wa kutafuta maji, kupunguza gharama yamaji ya kunywa na matumizi mengine ya nyumbani ambapo kabla ya mradi ndoo moja ya lita 20 ilikuwa ikiuzwa Shilingi 500 hadi 700 na sasa itakuwa shilingi 35 kwa ndoo moja.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji kutunza mradi huo na kuwadhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria watu watakaohujumu miundombinu ya mradi ili mradi huo uwe na manufaa kwa wananchi.

“Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga niwashukuru sana wadau wetu Shirika la ICS kwa kutekeleza mradi huu lakini pia shukrani za pekee ziende kwa shirika la Human Development Innovation Fund (HDIF) na UKaid kwa kukubali kuwa wafadhili wa mradi huu,niwaondoe hofu tu kuwa tutahakikisha tunautunza mradi huu”,aliongeza Talaba.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba akiangalia mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji mdogo wa Maganzo wilayani Kishapu wakati shirika la ICS lenye makao yake makuu nchini Uholanzi linalotekeleza shughuli za ulinzi wa mtoto (Child protection) katika nchi za Kenya na Tanzania likikabidhi mradi wa maji kwa serikali Julai 6,2018. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Injinia wa mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla unaotekelezwa katika mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu, Opita Tarcisius akimwelezea Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba kuhusu ujenzi wa mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 1.1.
Kulia ni Injinia Opita Tarcisius akielezea namna wananchi wanavyotumia vifaa vya kuwawezesha kununua maji kwa njia ya mtandao (Tags) kwenye vituo vya kuchotea maji ambavyo vina mfumo wa nishati ya jua (solar power).
Injinia Opita Tarcisius akionesha kifaa cha kununulia maji kwa njia ya mtandao (tag) kwenye vituo vya kuchotea maji.
Wadau wa maji wakiwa katika mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mtaa wa Majimaji kata ya Maganzo wilayani Kishapu.
Mashine ambayo mtumiaji wa maji hugusisha kifaa chake cha kununulia maji 'tag' kisha maji huanza kutoka.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akiwashukuru wadau wa maji shirika la ICS, Susteq na HDIF kwa ufadhili wa shirika la UK aid kufanikisha ujenzi wa mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla ambao utakuwa mkombozi kwa wananchi kwa kuwapunguzia gharama za maji na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Injinia wa Maji wilaya ya Kishapu, Lucas Said akielezea namna serikali ilivyoshirikiana na wadau katika kufanikisha ujenzi wa mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika Mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu.
Kijana Jamal Juma akigusisha kifaa cha kununulia maji kwa njia ya mtandao (Tag) kwenye mashine iliyopo katika kituo cha kuchotea maji katika mtaa wa Majimaji kata ya Maganzo wilayani Kishapu
Mwakilishi wa Meneja Mkazi wa shirika la ICS Tanzania, Peter Matyoko akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla (sustainable prepaid water meter system project) unaotekelezwa katika mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu.
Makamu Mkuu wa Mfuko wa HDIF, Joseph Manirakiza akizungumza wakati wa hafla ya zoezi la kuikabidhi serikali ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla unaotekelezwa na shirika la ICS katika mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu kwa ufadhili wa shirika la UK Aid kupitia Human Development Innovation Fund (HDIF).
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza wakati wa kupokea mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla unaotekelezwa na shirika la ICS katika mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu.
Kushoto ni Makamu Mkuu wa Mfuko wa HDIF, Joseph Manirakiza,katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Susteq na Injinia wa mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji mdogo wa Maganzo na kijiji cha Masagala wilayani Kishapu, Opita Tarcisius wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba.
Kushoto ni Mwakilishi wa Meneja Mkazi wa shirika la ICS Tanzania, Peter Matyoko akimkabidhi Makamu Mkuu wa Mfuko wa HDIF, Joseph Manirakiza nyaraka za mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala ikiwa ni ishara ya kukabidhi mradi huo. Makamu Mkuu wa Mfuko wa HDIF, Joseph Manirakiza ndiye aliyekabidhi mradi huo kwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Kulia ni Makamu Mkuu wa Mfuko wa HDIF, Joseph Manirakiza akikabidhi nyaraka za mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala kwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba akikabiidhi nyaraka za mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala kwa Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Injinia Lucas Said.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Injinia Lucas Saidakikabiidhi nyaraka za mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala kwa Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Maganzo (MAGAWASA), Rehema Abel.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Maganzo (MAGAWASA), Rehema Abel akizungumza baada ya kukabidhiwa mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala.
Meneja rasilimali watu KASHWASA Denis Mlingwa akiwasisitiza wananchi kutunza miundo mbinu ya maji na kuwafichua watu wanaohujumu miundombinu hiyo.
Meza kuu wakifuatilia matukio yaliyokuwa yanaendelea.
Diwani wa kata ya Maganzo Lwinzi Kidiga akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi endelevu wa maji kwa malipo kabla katika mji wa Maganzo na kijiji cha Masagala.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Boniface Butondo akiwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili miradi hiyo idumu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Maganzo Charles Manyenye akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi wa maji ambapo aliahidi kushirikiana na wananchi kutunza mradi huo kwa nguvu zote.
Wakazi wa Maganzo wakifuatilia matukio yaliyokuwa yanaendelea.
Wadau wa maji wakiwa katika eneo la tukio.
Wakazi wa Maganzo wafuatilia matukio yaliyokuwa yanajiri.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527