Wednesday, July 11, 2018

ENGLAND ISIPOMKABA MODRIC IMEKWISHA

  Malunde       Wednesday, July 11, 2018

England kama inataka kuifunga Croatia leo katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Dunia ili kutinga fainali, basi haina budi kufanya kazi ya ziada kumzuia kiungo bora kabisa duniani.

Mchezaji wa zamani wa Tottenham, Luka Modric. Ni mchezaji tofauti na ni wachache wenye uwezo kama wa mchezaji huyo, na wako wachache sana wenye kipaji kama alicho nacho Modric. 

Inaelezwa kuwa mara ya kwanza mchezaji huyo alionekana kipaji chake ni wakati timu ya Croatia ilipocheza dhidi ya England na kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2006 huko Zagreb.

Nilikuwa katika benchi usiku huo, na ndio nikasikia Spurs walikuwa wakitaka kumsajili na nilifikiria mwenyewe, sababu za timu hiyo kutaka kumsajili mchezaji huyo. Nilipojiunga na Tottenham mwaka 2008 nikiwa na umri wa miaka 22, tulikuja kuwa marafiki wa karibu na wakati huo tayari nilikuwa kiongozi, alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya nchi yake. Kiwango chake hakikutarajiwa na wengi, lakini kama mchezaji alikuwa na mambo mengi ya kushangaza katika kiwango chake.

USHINDI USHINDI

Mambo ambayo yamemfanya Modric kuonekana kuwa tishio kubwa kwa England katika mchezo huo wa leo Jumatano usiku, sio tu mtazamo wake, ila ni uwezo wake wa kutumia miguu yote miwili.

Ndio, na jinsi anavyoweza kutumia mwili wake wakati akiwa na mpira na amekuwa akitumia sehemu kubwa kumfanya kuwa mwanasoka wa aina yake na kuendelea kuwa na kiwango cha juu wakati wote. Luka wakati wote amekuwa akihitaji mambo mengi kutoka kwa wenzake na wakati fulani katika mchezo na wakati fulani amekuwa akilitegemea kundi, hata wakati wa miaka yake ya awali pale Tottenham. Baadhi ya wachezaji wabunifu wamekuwa wakitoka mchezoni wanaposhindwa kwenda katika njia yao, lakini hilo haliko kabisa kwa Luka.

Anahisia kali kuhusu soka na yuko makini sana awapo uwanjani. Huwa na hasira na hutaka ujue kama hajafurahia kitu fulani. Ni vigumu kuchukua mpira kwake na mpira unakwenda jinsi anavyotaka yeye. Nje ya kiwanja, ni mtu wa kawaida, na katika mazoezi huwa sawa na anavyokuwa katika mechi na huwa mtulivu sana wakati huohuo. Mara nyingi amekuwa akilalamikia maamuzi ya mwamuzi na kubishana na wachezaji wenzake, amekuwa akibishana nasi kuhusu aina ya ushangiliaji ushindi. Wakati wote akiwa mchezoni mawazo yake ni ushindi, ushindi, ushindi tu, huwa awazi kitu kingine zaidi ya ushindi.

HALI INAPOKUWA NGUMU

Wakati Luka alipokuja Tottenham alikuwa akicheza namba 10, lakini alicheza kwa chini zaidi, na upande wa kushoto au kulia pia. Kila nafasi anayocheza amekuwa makini katika jukumu lake, kwa sababu amekuwa na nidhamu ya ulinzi mchezoni na kamwe huwa haogopi kabisa changamoto, lakini kikubwa anachotaka kufanya kuwa na mpura na kuwajibika vilivyo uwanjani.

Napenda kucheza katika nafasi ya kiungo pamoja na Luka katika klabu ya Spurs na moja ya mambo niliyokuwa nayapenda sana ni jinsi alivyokuwa na akili pale anapokuwa katika mazingira magumu katika kiungo. Ukweli, anavyobanwa zaidi, ndio anakuwa yuko fiti zaidi na kucheza vizuri zaidi. Luka huwa na furaha pale anapopokea mpira sehemu yoyote, wakati wachezaji wengi wa viungo huwa na sehemu zao wanazofurahia kupeleka mipira.

Itakuwa vigumu sana kwa England kumzuia Luka katika mchezo huo wa leo Jumatano kwa sababu ni mwepesi na mwenye kasi zaidi ya wengi wanavyofikiria, na ana nguvu pia. Kwa mchezaji ambaye ana futi tano na inchi sita tu, kuweza kunyumbulika namna ile, sijawahi kuona katika maisha.

KWANINI MODRIC HASIFIWI?

Sasa ni miaka sita tangu Modric aondoke katika klabu ya White Hart Lane na kujiunga na Real Madrid – na tangu wakati huo amezidi kuwa bora zaidi. Ukimwangalia akicheza, ni wazi kijana huyo anaweza kubadilisha mchezo wake wowote na kufanya mambo yakatokea hasa sehemu ya kiungo, kutokana na uwezo wake alionao. Mchezaji huyo ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mara nne akiwa na Real Madrid, na sifikiri kama mchezaji huyo anapewa sifa anazostahili kwani wengi wanamchukulia poa tu.

Na hiyo labda inatokana na kutofunga mabao mengi na ndio maana hapati sifa inayostahili kutokana na uwezo wake mkubwa alionao uwanjani, lakini katika kipindi chote cha uchezaji wake hajawahi kufunga mabao mengi, kitu ambacho wengi wanakitumia kuamua uzuri wa mchezaji. Nafikiri ni tofauti na wachezaji wenzake wa Real Madrid kama Toni Kroos, Mhispania Andres Iniesta au wengine wa Croatia, Ivan Rakitic, Luka ni mchezaji mwenye kuibeba timu na mwenye uwezo wa kubadili mchezo wakati wowte anapotaka.

WAKONGWE CROATIA

Timu ya taifa ya Croatia inabebwa na wachezaji wake wakongwe, hasa katika safu ya kiungo kama akina Modric, Rakitic, Ivan Perisic na Ante Rebic – unaweza kusema kuwa ni mchezaji bora katika mashindano haya. Unaweza kuongeza wachezaji waliocheza katika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, kama akina mshambuliaji wa Juventus, Mario Mandzukic na yule wa Liverpool, beki Dejan Lovren, na unaweza kuona kwa nini wanafanya vizuri sana.

Presha kwa Luka sio tatizo kwake, ingawa hata wakati wa ujana wake, huko Croatia, alikuwa akichukuliwa kama mtu tofauti, alikuwa kama nyota ajaye kama walivyokuwa akina Zvonimir Boban na Robert Prosinecki. Sasa amekuwa mchezaji mkubwa Croatia na mwenye kutegemewa sana kwa sasa na ni tumaini la taifa lake.

Kukabiliana na presha hiyo kamwe hawezi kushtuka, na alionesha jinsi alivyo ngangari kiakili wakati wa hatua ya 16 bora timu yake iliposhinda dhidi ya Denmark. Alikosa penalti katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza lakini bado alikuwa mtulivu na kufunga wakati wa mikwaju mitano mitano ya penalti.

Hilo halikuwashangaza wengi. Kwani anajulikana uimara wake kwa sababu sio aina ya mchezaji anayekwenda majukumu yake. Croatia ina lundo la wachezaji wenye uzoefu na vipaji huku suala la kucheza kwa moyo likiwa halina mjadala, kwani timu hiyo inajua kupambana huku timu hiyo iliyotinga kwa mara ya pili nusu fainali katika historia yake, ina mapungufu kidogo.

Croatia imekuwa timu pekee ya pili kufanikiwa katika mikwaju ya penalti ikifuata nyayo za Argentina mwaka 1990, wakati walipoifunga Urusi 4-3 Jumamosi wakifuatiwa na ushindi dhidi ya Denmark katika raundi iliyotangulia. Wachezaji 14 wa kikosi cha Croatia wanacheza soka katika ligi tano kubwa Ulaya, kama England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa, ambao ni Luka Modric na Mateo Kovacic wanacheza Real Madrid, Ivan Rakitic yuko Barcelona na Mario Mandzukic yuko Juventus. Wakati Croatia walipotinga kwa kishindo hatua ya 16 bora wakiwa na pointi tisa baada ya mechi tatu, walianza kuonekana kuwa ni timu ya ushindani.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post