Wednesday, July 4, 2018

ALIYESIMAMISHWA KAZI NA MWIGULU KWA WARAKA WA KKKT AREJEA KAZINI

  Malunde       Wednesday, July 4, 2018
WIKI tatu baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba kuutangazia umma kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vyama vya Kijamii, Marlin Komba amesimamishwa kazi, imefahamika kuwa mtumishi huyo alisharejea kazini.


Juni 8, Dk Nchemba aliitisha mkutano na waandishi wa habari wizarani jijini Dar es Salaam na kutangaza kumsimamisha kazi Komba kutokana na barua yake aliyoiandika akilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), pamoja na mambo mengine, kufuta Waraka wa Pasaka wa maaskofu.


Katika mkutano huo, Dk Nchemba ambaye ameachwa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyotangazwa Jumapili iliyopita, alisema barua hiyo ni batili na haina baraka za Serikali na kwamba, ufuatiliaji ulionyesha ina mkanganyiko wa anuani na angefuatilia kujua ni nani aliyeiandika.


Komba jana alikuwapo miongoni mwa viongozi wa wizara ambao walimpokea Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliyeapishwa juzi na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo.


Baada ya mapokezi, Komba na viongozi wengine wa wizara walikuwa na kikao na waziri huyo.


Alipotafutwa kuzungumzia kurejea kwake kazini, Komba hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.


Hata hivyo, habari zinasema Komba alirejeshwa kazini baada ya utaratibu wa utumishi wa umma kufuatwa.


Awali, baada ya barua hiyo ya Msajili kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Juni 6, si waziri, wizara au msemaji wa Serikali aliyekubali kuizungumzia, lakini katibu mkuu wa KKKT alithibitisha kuipokea.


Waraka wa KKKT uliotolewa Machi 24 na uliosainiwa na maaskofu 27 ulizungumzia hali ya kiuchumi, ukipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kukusanya kodi, umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika mikakati ya maendeleo, utawala bora, demokrasia ya vyama vingi, usalama wa raia na masuala mengine mtambuka.


Barua, ambayo ilisainiwa na Komba kwa niaba ya msajili, ilisema chombo kilichotoa waraka huo hakitambuliwi kisheria na kwamba ulizungumzia masuala yaliyo nje ya malengo ya kanisa hilo na kutoa siku 10 kwa mkuu wa KKKT kuufuta waraka huo.


Hata hivyo, Dk Nchemba akiizungumzia alisema, “Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao. Nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na wasifanyie kazi taarifa hizo.”
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza wakati wa kikao cha viongozi wakuu wa wizara hiyo,Waziri Kangi Lugola(watatu kulia), Katibu Mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu (wapili kulia), Naibu Katibu Mkuu, Ramadhani Kailima(wakwanza kulia),aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Balozi Hassan Simba Yahaya(wapili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vyama vya Kijamii, Marlin Komba(wakwanza kushoto).Kikao hicho kimefanyika jana,jijini Dar es Salaam.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post