WAFANYABIASHARA WALILIA SOKO MANYOVU KIGOMA

Changamoto ya ukosefu wa soko katika kijiji cha Manyovu kata ya Munanila wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma, imekuwa kero ya muda mrefu ambayo imesababisha wafanyabiashara wengi wa eneo hilo kukimbilia Kasulu na mikoa mingine kuendeleza biashara zao hali inayosababisha kushuka kwa mapato katika Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Kigoma wananchi na wa fanyabiashara wa Manyovu ,walisema soko litakapojengwa watapata faida kubwa raia wa Burundi wamekuwa wakija Tanzania na kwenda kuchukua bidhaa katika wilaya ya Kasulu kwa kuwa Manyovu hakuna soko ingawa wananchi wana muamko wa kufanya biasha hivyo soko likijengwa itasaidia pia hata kuongeza pato katika wilaya na wananchi wote.

Azalia Ashery alisema wao kama wafanya biashara wa mazao ya ndizi na nanasi pamoja na vyakula vingine wanapata shida wanalazimika kuuzia biashara zao juani na mvua kuwanyeshea, hali inayosababisha mazao yao kuharibika na kupata hasara.

Naye Jackson Hemana alisema wafanyabiashara wengine wanalazimika kuuzia mazao yao shambani kutokana na ukosefu wa soko ambapo wanalazimika kuuza kwa bei ya chini kwa kuwa hakuna mahali watakapokwenda kuuzia.

Alisema endapo serikali itajenga jengo la soko itawasaidia sana wakulima kuinuka na kufanya biashara pamoja na kuinua wilaya ya Buhigwe kwa kuwa eneo hilo ni eneo maarufu kwa wakulima wa kahawa,ndizi , nanasi na mazao mengine ya chakula na biashara hivyo yatapata soko na kuinua uchumi wa Watanzania.


Akizungumza ofisini kwake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Brigedia Jenerali Marko Gaguti alisema kufuatia changamoto hiyo wao kama viongozi wa wilaya walishirikiana na kuandaa andiko la kuomba fedha Serikalini kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa litakalowakutanisha wananchi wa Burundi na Tanzania kufanya biashara katika soko la kimataifa ambalo litajengwa mpakani.

Alisema mradi huo umekubaliwa na hatua za awali zimekwisha kamilika ambapo Serikali kuu imetoa fedha shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya Ujenzi wa soko lenye Ghorofa moja litakalo kuwa na Ofisi 300 na maeneo ya vibanda vya wazi 500 na ujenzi utaanza mwaka wa fedha 2018-2019 na Julai mwaka huu watatangaza tenda ya awali na ujenzi utatumia mwaka mmoja.

"Sababu Kubwa ya kuuweka mradi huu Manyovu katika wilaya ya Buhigwe eneo hilo ni eneo maarufu kwa wilaya hii na mkoa kwa ujumla linalowakutanisha wafanyabiashara wengi kutoka nchi za jirani kutokana na mpaka huo kutumiwa na watu wengi ,soko hilo litakapokamilika litatoa chagizo kubwa kwa wananchi wa Buhigwe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kupata fursa ya biashara na kuongeza pato katika Halmashauri ya wilaya hiyo", alisema Brigedia Jenerali Gaguti.

Aidha aliwaomba wananchi washiriki kwa pamoja katika ujenzi wa soko hilo pamoja na usimamizi ili malengo ya serikali ya kukamilisha mradi huo unaotarajiwa kuingizia kiasi cha shilingi milioni 230 kwa halmashauri hiyo ukamilike kwa wakati ili kuongeza ukusanyaji wa mapato katika halmashauri.

Diwani wa Kata ya Munanila Baraka Lupori alisema anaishukuru serikali kwa kuweka mradi mkubwa wa soko katika eneo hilo ambalo lilikuwa kilio kikubwa kwa wananchi wa wilaya ya Buhigwe na kata hiyo ambapo wafanya biashara wengi wa eneo hilo walikimbia kutokana na kukosa soko hali iliyosababisha kushuka kwa mapato kusababisha kata hiyo kukusanya kiasi cha shilingi milioni tatu tu kwa mwezi.

Alisema Munanila ni mpaka unaokutanisha wananchi wa nchi tatu za Burundi, Rwanda na Congo, na wananchi wengi wa Burundi wanategemea bidhaa za chakula kutoka katika vijiji vya Manyovu na wilaya ya Buhigwe kwa ujumla soko hilolitakapo kamilika litasaidia wafanya biashara wengi walioondoka Manyovu na kuhamia maeneo mengine kwa ajili ya kuendeleza biashara zao kurejea na kufanya biashara na kipato cha halmashauri na wananchi kitaongezeka.

Na Rhoda Ezekiel Kigoma




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527